Wataka mabadiliko sheria wanyamapori

08Dec 2021
Salome Kitomari
Dar es Salaam
Nipashe
Wataka mabadiliko sheria wanyamapori

WATAALAMU wa uhifadhi na wanyamapori wamesema bila kufanya mabadiliko ya sera na sheria za wanyamapori, itakuwa vigumu kusaidia wanyama wanaokosa maji na malisho kwenye maeneo yaliyohifadhiwa kama Hifadhi za Taifa.

Meneja wa Sekta Binafsi wa Shirika lisilo la kiserikali la RTI linalotekeleza mradi wa Tuhifadhi Maliasili Activity kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID), Dk. Elikana Kalumanga, alisema hayo hivi karibuni wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari juu ya uandishi wa habari za wanyamapori na uhifadhi.

Kwa Tanzania mradi huo wa miaka mitano unatekelezwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET).

Akiwasilisha mada ya mapito ya wanyama na hali ilivyo kwenye maeneo hayo, alisema kutokana na hali ya ukame wa muda mrefu uliosababisha wanyama au kuteseka kwa kukosa maji, kunaibua mjadala wa namna wanavyoweza kusaidiwa.

“Sera na sheria hazijaeleza kwa uwazi kuwa inapotokea ukame nini kifanyike. Mathalani kwenye hifadhi za taifa ambako asili inapaswa kuachwa hairuhusiwi kuingiza au kutoa chochote. Je, maji yapelekwe kwenye mabwawa na yatoke kwenye bajeti ipi? Kwa sasa tunaona kunaongezeko la migogoro kwa kuwa wanyama wanatoka maeneo yao kutafuta malisho,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Kalumanga, Zimbabwe na Namibia zimetengeneza mahali kuweka chumvi maalum inayotumiwa na wanyama ambayo hupelekwa na kuongezwa kila inapokwisha na kwamba kwa nchini inahitajika mjadala wa kina kwa kuwa kwa sasa maeneo ya wazi ambako wanyama walikuwa wanapata mahitaji muhimu kumefungwa na shughuli za binadamu.

“Kuna shoroba hazipitiki tena. Kuna ambazo zikiwahiwa zitapitika mfano kwenye maeneo ya wafugaji hakuna shida. Tatizo liko maeneo ya wakulima mfano kijiji cha Mang’ola wanakolima vitunguu kumekuwa na migogoro mingi. Tulichelewa kusema kuna shoroba na zina ukubwa gani ili tuzihifadhi,” alisema.

Dk. Kalumanga alisema kufungua shoroba si ombi bali ni lazima ili wanyama waendelee na safari zao, waishi kwa sasa kwasababu ya ukame wanateseka kwa kuwa hawapati majani, maji na madini muhimu.

“Wako walio na mimba ambayo inahitajika kukuzwa kwa madini fulani lakini wanapokwenda eneo la mtawanyiko kupata mahitaji hayo wanakutana na shughuli za kibinadamu. Wengine ni utaratibu wao kuzalia eneo fulani ambalo kwa wakati huo huwa na majani machanga kwa ajili ya ndama wao. Sasa wanashindwa kuzaa kwa kuwa hakuna majani. Mfano nyumbu anaweza kushikilia mimba kwa miezi mitatu kama anaona mazingira siyo salama kwa ndama,”alisema.

Alisema viumbe wanatakiwa kusafiri kutoka eneo moja kwenda jingine na kwamba shoroba zinachangia maendeleo ya uhai hivyo binadamu waache kuyatazama kama maeneo yao bali yetu.

Kwa mujibu wa Dk. Kalumanga, shoroba ya Kwakuchinja ilikuwa na ukubwa wa kilomita 21, lakini kwa sasa zimebaki mbili na imewezekana baada ya wananchi kushirikishwa na kuona umuhimu wa utalii na uhifadhi.

Meneja Tathmini na Ufuatiliaji wa RTI, John Noronha, akiwasilisha mada ya kinachochochea migogoro baina ya binadamu na wanyama, alisema kwa kipindi cha mwaka 2012 hadi 2019 zaidi ya watu 1,069 walikufa kwa kushambuliwa na wanyama huku 642 wakijeruhiwa.

Ekari 41,404 ziliharibiwa na mifugo 792 ililiwa na wanyama huku Sh. bilioni 4.67 zililipa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa na mali.

Habari Kubwa