Wataka mazingira wezeshi uchaguzi mitaa

23Oct 2019
Elizaberth Zaya
Dar es Salaam
Nipashe
Wataka mazingira wezeshi uchaguzi mitaa

CHAMA cha Wasioona Tanzania, kimeiomba serikali kuweka mazingira wezeshi kwa kundi hilo ili nalo lishiriki ipasavyo kwenye uchaguzi wa serikali za mitaa.

Uchaguzi wa viongozi wa serikali za mitaa unatarajiwa kufanyika Novemba 24, mwaka huu.

Wakizungumza na Nipashe jana kwa nyakati tofauti, baadhi ya viongozi wa chama hicho walisema mpaka sasa mfumo wao wa kupiga kura kuwachagua viongozi katika ngazi mbalimbali bado si wa siri.

Mratibu wa Wanawake na Watoto wa Chama hicho, Rehema Daruweshi, alisema katika uchaguzi mbalimbali wamekuwa wakishiriki lakini bado uamuzi wa kuamua kiongozi wanayemtaka uko mikononi mwa watu wengine.

"Unajua sisi ambao hatuoni bado hatuwezi kusema tunamchagua kiongozi tunayemtaka. Maamuzi yetu bado yako mikononi mwa watu ambao hasa ni ndugu zetu ambao wanakuwa wametusindikiza kwenda kupiga kura,” alisema.

"Kwa mfano mimi nakwenda na mwanangu ananisindikiza kwenda kupiga kura. Nikifika katika sanduku la kura na mwelekeza amchague kiongozi ninayempenda, anaweza kuniitikia. Lakini tukumbuke kwamba na yeye ana chaguo la mtu anayemtaka na mwisho wa siku yeye ndiye anayeona na ndiye mwenye uamuzi wa mwisho pale katika kuweka wino. Naweza kumwelekeza anichagulie kiongozi A lakini kwa mapenzi yake na kwa kuwa sioni, akachagua kiongozi B."

Kutokana na mazingira hayo, alisema ni vyema serikali ikaandaa mazingira ambayo hayatamlazimu mtu asiyeona kumhusisha mtu wa pili katika kupiga kura mwenyewe pasipo usaidizi.

Naye Mratibu wa Maendeleo ya Vijana na Chipukizi wa chama hicho, Kiongo Itambu, aliiomba Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuanzisha utaratibu maalum wa kuwafikia watu wenye ulemavu kupitia katika vyama vyao kwa ajili ya kuwapatia elimu ya uraia.

Habari Kubwa