Wataka ofisa polisi atumbuliwe kwa rushwa

22Oct 2017
Na Mwandishi Wetu
Nipashe Jumapili
Wataka ofisa polisi atumbuliwe kwa rushwa

MWANAKIJIJI Nyambale wilayani Biharamulo mkoa wa Kagera, Bilatwa Mabuga, ametaka ofisa wa polisi atumbuliwe kwa kuomba rushwa na kunyanyasa wafugaji.

Mwanamama huyo, aidha, ameilalamikia Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wilayani humo kushindwa kumkamata ofisa huyo wa polisi (jina tunalo) wa kituo cha Lusaunga anayedai alimuomba rushwa ya Sh 1,000,000 .

Alidai, aliombwa fedha hizo ili polisi iwaachie ng’ombe 20 wa mwanamke huyo waliokamatwa wakati wakisafirishwa kwenda mnada wa Katoke .

Akizungumza na gazeti hili katika Kijiji cha Kabumbilo alisema kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 22 mwaka huu wakati mwanae Pambano Luhumja, akisafirisha mifugo hiyo kutoka wilaya Kasulu mkoa wa Kigoma kwenda mnada wa Katoke wilayani Biharamulo

Alisema kuwa baada ya kufika katika Kijiji cha Lusahunga, mwanae alikamatwa na ofisa huyo wa polisi wa Lusahunga akimtuhumu kusafirisha ng`ombe bila kibali licha ya kuonyeshwa nyaraka za kusafirishia mifugo hiyo .

Mabuga alisema kuwa baada ya kupigiwa simu na mmewe Luhumja Mkama kuwa ng`ombe wamekamatwa alilazimika kwenda kituo cha polisi akiwa ameambatana na jirani yake ambaye aliwakuta ng`ombe hao na mwanawe wakiwa chini ya ulinzi .

Aliongeza kuwa alipotaka kufahamu sababu ya kukamatwa mwanae pamoja na mifugo hiyo polisi huyo alimtaka atoe 1,000,000 ili amwachie mwanae pamoja na mifugo hiyo na kwamba Septemba 24 aliporudi kituoni hapo ofisa huyo , alimtaka atoe Sh. 300,000 ili amuachilie huru mwanae pamoja na mifugo kabla ya kuwapeleka mahakamani .

Mwenyekiti wa Kitongiji cha Kibale Kijiji cha Kabumbilo wilayani Biharamulo, Paulo Mussa, aliyehusika kumdhamini mtoto wa mama huyo, alithibisha kuwepo kwa tukio hilo na kusema kuwa ofisa wa Lusahunga amekuwa kero kubwa kwa wananchi kutokana na tabia yake ya kuwabambikiza kesi.

Alidai kuwa wananchi wanasingiziwa makosa mbalimbali kwa lengo la kujipatia fedha kwa maslahi binafisi na hivyo kuiomba serikali kumuondoa askari huyo haraka .

“Amekuwa kero tena akijihusisha na rushwa na kubambikiza kesi wananchi kitendo ambacho ni hatari na amekuwa tatizo kwa wananchi tunaomba ashughulikiwe kwa mujibu wa sheria na Takukuru,” alisema Mussa.

Aidha, Katibu wa Chama Cha Mapinduzi, CCM wilayani Biharamulo mkoani Kagera, Joyce Massi, alikiri kupokea malalamiko hayo kutoka kwa wafugaji hao wakidai kuombwa ruhwa na ofisa mmoja wa kituo cha Polisi Lusahunga baada ya kukamata mifugo yao.

Wanyama wanakamatwa wakati wakiisafirisha kutoka wilaya ya Kasulu mkoa wa Kigoma kwenda minadani.

Alisema kuwa baada ya kuwasikiliza malalamiko walionyesha nyaraka halali za kusafirishia mifugo hiyo na kubaini kuwa zinahitajika hatua za kisheria na kuwapeleka kwenye ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Biharamulo .

Kamanda wa Takukuru wilayani Biharamulo Hassan Mossi, alikiri kupokea malalamiko kutoka kwa wafugaji huku akigoma kuzungumzia zaidi kwa madai kuwa uchunguzi unaendelea.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kagera Augustino Ollomi, akizungumza na gazeti hili jana kwa njia ya simu alikiri askari wake kutuhumiwa kuomba rushwa na kwamba hawezi kulizungumzia zaidi kwa kuwa liko Takukuru .

Habari Kubwa