Wataka picha ya Magufuli kwenye noti

08Apr 2021
Nebart Msokwa
MBEYA
Nipashe
Wataka picha ya Magufuli kwenye noti

SERIKALI imeombwa kuchapisha noti mpya zenye picha ya aliyekuwa Rais wa  Tanzania, Hayati Dk. John Magufuli, kwa ajili ya kumbukumbu na kuenzi kazi nzuri alizolifanyia taifa wakati wa uhai na uongozi wake.

Pia imeombwa kuchapisha noti zingine zenye picha ya Rais wa sasa, Samia Suluhu Hassan, ili iwe kumbukumbu yake ya kuwa Rais wa kwanza mwanamke wa Tanzania.

Ombi hilo lilitolewa juzi jijini Mbeya na Kamati Tendaji ya Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za kifedha na Huduma na Ushauri (TUICO) wakati wa kuhitimisha siku 21 za maombolezo ya kitaifa ya kifo cha  Hayati Dk. Magufuli.

Akizungumza wakati kutia saini kitabu cha maombolezo juzi, Katibu wa TUICO Mkoa wa Mbeya, Melboss Kapinga, alisema kamati hiyo inapendekeza picha ya Hayati Magufuli ichapishwe kwenye noti ya Sh. 5,000.

“Lakini pia tunapendekeza ikiwezekana ichapishwe noti ya Sh. 20,000 au 6,000 na kuwekwa picha ya Rais Samia ili iwe kumbukumbu kwake kutokana na kuwa Rais wa kwanza mwanamke katika nchi yetu,” alisema Kapinga.

Mwenyekiti wa TUICO Mkoa wa Mbeya, Luka Mwasimba, alisema Dk. Magufuli katika uhai wake, alifanya mambo makubwa ya maendeleo ambayo yanatakiwa kuwekewa kumbukumbu ili hata vizazi vijavyo vimkumbuke.

Alisema kamati hiyo inapendekeza picha yake iwekwe kwenye noti ya Sh. 5,000 kwa sababu ni miongoni mwa noti kubwa katika fedha za Kitanzania huku akidai kuwa picha ya Rais Samia inapendekezwa iwekwe kwenye noti mpya kabisa ambayo haijawahi kuchapishwa.

“Katika historia ya taifa letu hatujawahi kuwa na Rais mwanamke, hivyo tunapendekeza picha yake iwekwe kwenye noti mpya kabisa ambazo tunapendekeza iwe 20,000 au 6,000,” alisema Mwasimba.

Nao baadhi ya wajumbe wa Kamati Tendaji ya TUICO Mkoa wa Mbeya walieleza namna ambavyo watamkumbuka hayati Dk. Magufuli huku wakimwombea heri Rais Samia ili aliongoze vyema taifa.

Mmoja wa wajumbe hao, Alex Kilamlya, alisema Hayati Dk. Magufuli alifanya mambo mengi wakati wa uhai wake, hivyo anatakiwa kuenziwa kwa namna yoyote ile ikiwamo Watanzania kufanya kazi kwa bidii.

Alisema kiongozi huyo ameliacha taifa likiwa limefikia hatua ambayo ni nzuri na kila mmoja anatakiwa kuhakikisha analifanyia taifa mambo mazuri ikiwamo kulipa kodi kwa ajili ya kuendeleza miradi ya kimkakati iliyoanzishwa pamoja na uendeshaji wa shughuli za Serikali.

Naye Anna Mwakyembe alisema ana uhakika Rais Samia ataliendeleza taifa kutokana na kwamba alikuwa anafanya kazi na Hayati Dk. Magufuli na kutokana na hali hiyo, ana uwezo na uzoefu wa kutosha wa kushika nafasi hiyo.

Aliwataka Watanzania kuendelea kumpa ushirikiano Rais Samia na serikali yake ili aendeleze miradi ambayo waliianzisha pamoja na hayati Dk. Magufuli.

 

Habari Kubwa