Wataka ulinzi, kuthaminiwa kwa wasio na ajira rasmi

09Mar 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Wataka ulinzi, kuthaminiwa kwa wasio na ajira rasmi

KATIKA jitihada za kupigania haki za wanawake, asasi za mbalimbali za kiraia zimetangaza kampeni ya kitaifa ya kutambua mchango wa wanawake walio kwenye ajira zisizo rasmi, ili wathaminiwe na wapate haki zao.

Kampeni hiyo ilitangazwa jana jijini Dar es Salaam katika tamko la pamoja la mashirika ya kiraia yakiwamo Shirika la Wanawake Katika Sheria na Maendeleo Afrika (WiLDAF), Chama cha Wanasheria Wanawake (TAWLA) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (WLAC).

Mengine ni Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (Tucta) na mashirika ya kimataifa ya Action Aid Tanzania na Oxfam wakati wa Siku ya Wanawake Duniani.

“Tunatumia fursa hii Siku ya Wanawake Duniani kutambulisha rasmi kampeni yetu inayolenga kushawishi wanawake kupata ajira, kazi za staha na kuhakikisha huduma za kijamii kwa mwanamke zinapatikana”, lilisema tamko hilo lililosomwa na Anna Kulaya wa Wildaf.

Liliongeza kuwa ajira zisizo rasmi zinawanyima wanawake fursa ya kupata haki na stahiki za kazi kama mikataba inayozingatia saa za kufanyakazi, kutokuwa wanachama wa mifuko ya hifadhi ya jamii, bima ya afya, kunyimwa likizo za uzazi na za ugonjwa.

Aidha, watetezi hao walisema katika kampeni hiyo masuala ya upatikanaji wa huduma bora za kijamii kama ajira, afya na elimu zitapewa kipaumbele ili zimpunguzie mzigo mwanamke.

“Elimu ni kigezo muhimu cha kupata ajira, lakini kutokana na vikwazo kama mimba za utotoni wanawake wengi hawafikii elimu ya juu hivyo kusababisha idadi ndogo ya wanawake wenye ajira rasmi,” alisema Kulaya aliyewasilisha tamko hilo.

Kadhalika, malipo duni kazini ni tatizo linawaathiri wanawake kwa mujibu wa tamko. Kutokana na unyanyasaji imebainika kuwa licha ya baadhi ya wanawake kuwa na elimu inayolingana na wanaume hawapati malipo sawa. Wanawake wanapunjwa na sababu hazifahamiki.

Aidha, kampeni hiyo italenga kukomesha tatizo la ukatili na unyanyasaji wa kijinsia mahali pa kazi kwani imebainika kuwa wanawake wengi walioko kwenye ajira zisizo rasmi wanakabiliwa na changamoto hiyo ambayo inafumbiwa macho kwa miongo mingi.

“Waathirika hawana ujasiri wa kutoa taarifa za vitendo hivyo kwa hofu ya kupoteza ajira,” lilisema tamko hilo linalolenga kuwafikia wanawake mijini na vijijini.

Tamko liliongeza kuwa, wanaolengwa ni walioko kwenye sekta ya kilimo, biashara, ndogo ndogo, vibarua viwandani na migodni.

Aidha, wadau hao walitoa wito kwa serikali kutambua na kutoa haki kwa wanawake walio kwenye ajira zisizo rasmi ikiwa ni pamoja na likizo za uzazi, muda wa kunyonyesha, ulinzi dhidi ya unyanyasaji , mikataba ya kazi na malipo stahiki.

Aidha, wadau hao wanapendekeza serikali iboreshe miundombinu mijini na vijijini ili kuwapunguzia wanawake na mabinti mzigo wa kazi za kulea familia kwa kuwapatia huduma muhimu za maji, tiba na elimu ambazo zimekuwa changamoto kubwa.

Habari Kubwa