Wataka vikao kama JPM, wadau madini

27Jan 2019
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Wataka vikao kama JPM, wadau madini

SIKU tano baada ya Rais John Magufuli kukutana na wachimbaji na wafanyabiashara wa madini, wadau wametaka wizara, taasisi na idara za serikali kuwa na vikao vya mara kwa mara vya aina hiyo ili kubaini changamoto zilizoko katika sekta zao na kuzifanyia kazi.

WADAU WA MADINI WAITAKA WIZARA HUSIKA KUWEKA VIKAO MARA KWA MARA

Mkurugenzi wa kampuni ya kuchakata dhahabu ya Nyakato, Vaya Rajendra, ambaye hivi karibuni kampuni hiyo itaanza uchimbaji baada ya kupata vibali kutoka serikalini, aliomba ili sekta mbalimbali kutatua changamoto zilizopo kwenye maeneo yao, wadau waige kile kilichofanywa na Wizara ya Madini.

 

Rajendra alisema kitendo cha kuandaliwa kwa mkutano wa madini ambao Rais John Magufuli alitoa fursa kwa wadau kutoa madukuduku yao ili kubaini wapi wamekosea ni jambo zuri ambalo linatakiwa kuigwa na taasisi zingine za serikali.

 

“Kwa kuruhusu wadau kukaa pamoja mara kwa mara na wizara, idara au taasisi husika kutaifanya Tanzania kuongoza barani Afrika kwa ukuaji wa uchumi kwa sababu watajua changamoto zilizopo na kuzitatua tunamshukuru Rais kwa hatua hii,” alisema.

 

Rajendra mwenye uzoefu wa takriban miaka 40 kwenye uchimbaji dhahabu, alisema ziara zikifanywa kama alivyofanya Rais Magufuli mbele ya wadau wa madini, nchi itakuwa namba moja Afrika pasipo urasimu.

 

Aidha, alisema Wizara ya Maliasili na Utalii, Wizara ya Kilimo na Wizara ya Viwanda na Biashara zikifuata utaratibu huo wa kuhakikisha kila mara wanakutana na wadau wao watamrahishia kazi Rais Magufuli kuifikisha Tanzania kwenye uchumi wa kati wa viwanda.

 

"Dubai ni jangwa lakini kwa sababu ya sera zao nzuri na zisizo na ukiritimba, dunia nzima inatamani kuwa kama wao, tunaamini Tanzania ikifuata mfano huu itapiga hatua kiuchumi na kuwazidi wao,” alisema.

 

Kwa upande wake, Meneja wa Kampuni ya Madini ya Busolwa ya jijini Mwanza iliyoingia ubia na kampuni ya Nyakato, Mrisho Masebu, alisema tayari wameshatoa  zaidi ya ajira 290.

 

Alisema mtambo wa Misungwi unatarajiwa kukamilika Mei na kuanza kazi rasmi mwezi utakaofuata na kila siku wanategemea kuzalisha kilo 50 na tani moja ya makinikia na kupatikana kwa dhahabu safi itakayouzwa Dubai, Ulaya, Marekani na kwenye benki.

 

 

 

Habari Kubwa