Watakiwa kuwa na leseni uchimbaji madini ya ujenzi

03Dec 2019
Shaban Njia
KAHAMA
Nipashe
Watakiwa kuwa na leseni uchimbaji madini ya ujenzi

WACHIMBAJI wadogo wa madini ya ujenzi wilayani Kahama mkoani Shinyanga,wametakiwa kuwa na vibali/lesini ya uchimbaji wa madini hayo ili kuondokana na usumbufu unaoweza kujitokeza baina yao na maaofisa wa madini.

Ofisa madini wa Mkoani Shinyanga Mhandisi Joseph Kumburu akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi jana katika ukumbi wa Halmashauri ya Mji wa Kahama.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Ofisa Madini Mkoani Shinyanga Mhandisi Joseph Kumburu wakati akizungumza na wachimbaji wadogo wa madini ya ujenzi ya mchanga, kokoto na moramu na kuwataka kuacha kuchimba madini hayo kandokando mwa barabara na vyanzo vya maji.

Alisema kuwa kila mchimbaji anatakiwa kuwa na leseni ya uchimbaji wa madini na mchimbaji atakae baina kuendesha shughuli hizo bila ya kuwa na leseni, atachukuliwa hatua za kisheria kwa mujibu wa sheria ya madini ya mwaka 2010.

Alisema kuwa sheria ya madini ya mwaka 2010 kifungu namba 30 kilichofanyiwa marekebisho mwaka 2017 kifungu namba sita cha uwazi na uwajibikaji, nikosa kisheria kwa mtu yoyote kufanya shughuli za uchimbaji wa madini bila kuwa na leseni.

Pia Mhandisi Kumburu amewataka wachimbaji hao kulipa ushuru unaopatika kwenye madini hayo kwa wakati na sio kusubiria mpaka wafuatwe na maafisa madini,sambamba na kutochimba madini hayo kwenye maeneo ambayo hayajatengwa na serikali.

Wachimaji wadogo wa madini ya  ujenzi na wamiliki wa magari ya kubeba madini hayo wakimsikiliza Ofisa Madini Mkoa wa shinyanga Mhandisi Joseph Kumburu hayupo pichani.

“Hakikisheni kila mchimbaji wa madini ya ujenzi anakuwa na leseni ili kusije kuibuka malalamiko wakati tunapoaanza kufanya kazi zetu na hakikisheni wachimbaji hamchimbi madini kandokando ya barabara na pembezoni mwa vyanzo vya maji”alisema Mhandisi Kumburu.

Kwa upande wake Ofisa Afya na Mazingira kutoka Halmashauri ya Mji wa Kahamna, Johanes Mwebesya, alisema kuwa, Halmashauri kwa kushirikiana na Ofisa ya madini katika mji huo imetenga maeneo kwenye kata ya Wendele na Ngogwa kwa ajili ya uchimbaji wa madini hayo.

Alisema kuwa, kila mchimbaji mdogo anatakiwa kwenda kuendesha shughuli za uchimbaji wa madini hayo kwenye maeneo yametengwa na Halmashauri kwani itasaidia kutatua changamoto ya uharibifu wa mazingira kwa kuchimba madini kiholela.

Makamu Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa madini Mkoani Shinyanga (SHIREMA) Nicodemus Majabe, alisema, kwa mchimbaji wa madini atakae kwepa kulipa kodi za serikali watamchukulia hatua za kisheria kwanza kabla ya serikali hajamshughulikia.

Hata hivyo amewataka kuchimbaji kutochimba madini hayo kiholela na badala yake wachimbe kwenye maeneo yaliyotengwa kisheria nakuongeza hawatachukua jukumu la kumtetea mchimbaji yoyote atakaebainika kwenda kinyume na maagizo yaliyotolewa.

Habari Kubwa