Watakiwa kuacha unyanyapaa wagonjwa wa corona

28May 2020
Neema Emmanuel
MWANZA
Nipashe
Watakiwa kuacha unyanyapaa wagonjwa wa corona

Maofisa ustawi wa jamii wametakiwa kuondoa unyanyapaa, ubaguzi unaojitokeza katika kipindi hiki cha ugonjwa wa corona ngazi ya mtu moja moja,familia na jamii na wafanye utambuzi wa mahitaji kwa walio katika mazingira hatarishi na kutoa huduma ya msaada wa kisaikoojia na kijamii.

Hayo yamebainishwa na Mkurugenzi Msaidizi huduma za Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Rasheed Maftah wakati akifungua mafunzo ya siku tatu ya ushauri nasaha(PSS) yaliyofadhiliwa na Plan International Tanzania amesema mambo yanayopaswa kufanyika ili kuleta tija ni kufanya tathimini ya mahitaji na kuwaunganisha wateja na huduma zinazohitajika.

 

Amesema mafunzo hayo yametolewa kwa maofisa ustawi 50 hivyo jamii inatakiwa kuondolewa hofu ya ugonjwa huo, mipango kazi inatakiwa kuandaliwa na kuhakikisha wanatoa taarifa za utekelezaji katika ngazi ya mkoa na kutumia takwimu zinazopatikana kwa ajili ya kufanyia maamuzi ngazi ya Halmashauri sambamba kufanya kazi na wadau mbalimbali wanaotoa huduma ya ushauri nasaha.

 Pia amewataka watambue mafunzo hayo yana lengo la kuwezesha timu ya wataalam wanaotoa ushauri nasaha ngazi ya Halmashauri na kamati ya ulinzi wa mwanamke na watoto kufahamu jinsi ya kutoa huduma kwa ngazi zote katika kipindi hiki cha ugonjwa huo kwa ushirikiano wa Plan International Mwanza.

 “Napende kuwashukuru sana Plan International Mwanza kwa msaada huu wa kusaidia mafunzo kwa wataalamu wa Ustawi wa Jamii Halmashauri za Ilemela na Nyamagana ili waweze kutoa huduma hiyo katika kipindi hiki cha ugonjwa, pamoja na msaada mkubwa tunaopata, Ofisi Rais Tamisemi inahitaji huduma hizi ziwafikie jamii nzima yaani Halmashauri zote za Mwanza, hivyo tunaomba Plan International kuendelea kutanuka wigo katika Halmashauri Tano zilizobaki ili huduma hizi ziwafikie na walengwa wengine” amesema Maftah

 Kwa upande wake Meneja wa Kitengo kutoka Plan Internation Tanzania Dk. Majani Rwambali, amesema wameamua kutoa elimu kwa maofisa Ustawi hao wa Halimashauri ya Ilemela na Nyamagana ili kuwasaidia na kuwajengea uwezo kwa kuwa wao kwa sehemu kubwa  ndio wanafanya kazi bega kwa bega na wataalamu walio katika mahospitali kwa ajili ya tiba huku wakiipatia  jamii ushauri mbalimbali kuhusiana na afya zao na namna  gani wanaweza kuishi na kuimili maambukizi ya ugonjwa huo sambamba na utoaji wa elimu.

 Anaongeza kuwa watakapokuwa na uwezo wataweza kutoa tiba ya ubongo na mioyo na kuwaondolea hofu na kuweza kuendelea vyema hivyo wataendelea kushirikiana na serikali kwa kuwa wao ni wadau wao wakubwa pia aliwataka wadau wengine wajitokeza na kuisaidia serikali katika mapambano ya kuutokomeza ugonjwa huo.

 “Hitaji hili lilijitokeza wakati tulipokuwa tumejikita kununua vifaa vya kujikinga wakati huo huo tukiendelea  kutoa vifaa hivyo kama barakoa ,sanitizer ,groves na kuvigawa hapo ndipo likaja hitaji lingine kutoka kwa wadau wetu wakuu ambao ni serikali kwamba tumejielekeza zaidi katika kumwangalia mgonjwa anayefika hospitali lakini mgojwa huyo anaweza kupata ushauri utakaomjenga na kumuondolea hofu na akaweza kuendelea vizuri katika ugonjwa uliompata  kwa kupewa ushauri hivyo tumechukua hatua ya kusaidiana na vizara katika jambo hili kwa kuwafunda Maofisa Ustawi ” amesema Rwambali.

 Faith Lukindo ni Ofisa Ustawi wa Jamii, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Omary Nassoro Ofisa Ustawi Wilaya ya Nyamagana ni baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wanasema mafunzo hayo yana umuhimu na manufaa makubwa kwa sababu mwanzo walifanya kazi pasipo kupata mafunzo lakini baada ya mafunzo hayo wamepata uwezo na ujasiri wa kufanya kazi ipasavyo na kuwashushia hofu jamii na kuondokana na gonjwa hilo. 

Wameongeza kuwa wanao uelewa mzuri wa kuisaidia jamii na kutatua changamoto zao pia walitoa shukrani kwa Plan International na TAMISEMI kuwasaidia kupata mafunzo yenye kuleta chachu itakayoijenga nchi.

Habari Kubwa