Watalaam wa chuo cha Oxford watoa mafunzo kwa madaktari bingwa

15Jul 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Watalaam wa chuo cha Oxford watoa mafunzo kwa madaktari bingwa

WATALAAM kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu Oxford nchini Uingereza, wameanza kutoa mafunzo kwa madaktari bingwa wa damu, madaktari bingwa wa saratani na wauguzi jinsi kuhudumia wagonjwa wa saratani pamoja na wagonjwa watakaopandikizwa Uloto (Bone Marrow Transplant).

Mtaalam wa Tiba ya Magonjwa ya Saratani kutoka Hospitali ya Chuo Kikuu cha OXFORD nchini Ungereza, Finn Tysoe, akitoa mafunzo wa wataalam mbalimbali wa MNH leo.

Hatua hiyo ni mwendelezo wa maandalizi ya kutoa huduma ya upandikizaji Uloto kwa mara ya kwanza nchini, matibabu ambayo yalikua hayapatikani kutokana na kutokuwepo wataalamu au ukosefu wa vifaa vya kutolea huduma husika.

Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Kitengo cha Mafunzo, Ushauri na Utafiti,  Dk. Faraja Chiwanga, amesema mafunzo yameanza kutolewa MNH yanahusisha madaktari bingwa wa magonjwa ya damu na saratani 20 na wauguzi zaidi ya 30.

Alisema Juni mwaka huu, MNH ilipeleka watalaamu 11 nchini India katika Hospitali ya Apollo iliyopo Chennai kwa kipindi cha mwezi mmoja ili kujifunza kwa njia ya vitendo jinsi ya kufanya upandikizaji wa Uloto.

Baadhi ya wataalam wakifuatilia mafunzo ya jinsi ya kuwahudumia wagonjwa watakaopandikizwa ULOTO. Huduma hii inatarajiwa kuanza nchini mwishoni mwa mwa huu katika hospitali hii.

“Uwepo wa huduma hii utasaidia wananchi wengi kutibiwa nchini, kujenga uwezo kwa wataalamu wa ndani na itapunguza mzigo kwa Serikali kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa sababu gharama za kufanya upasuaji nchini zitashuka kufikia kiasi cha chini ya asilimia 50 kwa mgonjwa mmoja,”Dk. Chiwanga amesema.

Amesema wagonjwa wenye tatizo hilo waliokuwa wakipelekwa nje ya nchi na kutibiwa kwa gharama ya Sh. milioni 200, hivyo MNH mgonjwa itagharimia chini ya asilimia 50.

Habari Kubwa