Watalii waanza kuja Tanzania

22May 2020
Augusta Njoji
Dodoma
Nipashe
Watalii waanza kuja Tanzania

NDEGE ya kwanza iliyobeba watu saba wakiwamo watalii wanne kutoka Ugiriki ilitua jana katika Uwanja wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

Ndege hiyo imewasili zikiwa ni siku chache baada ya kutangaza kufungua kwa anga la Tanzania lililokuwa limefungwa kutokana na ugonjwa wa corona.

Sambamba na hilo, Mei 28, mwaka huu, Tanzania inatarajia kupokea ndege nyingi zaidi ikiwamo za watalii.

Akizungumza jana na waandishi wa habari, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Isack Kamwelwe, alisema ndege hiyo ilitua uwanjani saa tatu asubuhi.

“Ndege iliyotua ilikuwa na watalii wanne na crew ya watu watatu na wametua tayari, wamepokelewa na wamekwenda kuangalia wanyama,” alisema.

Aidha, alisema anaratiba ya ndege zitakazofanya safari zake kuja Tanzania na booking zimejaa, huku akisisitiza ifikapo Mei, 28, mwaka huu ndege nyingi zaidi zitatua ikiwamo zilizobeba watalii.

“Yapo mashirika ya ndege yalishajiandaa kama Emirate, Ethiopia, KLM na kwa upande wa zitakazofanya safari za mizigo tulianza na Rwanda Airline kuanza kubeba minofu ya samaki, leo (jana) tumeongeza ndege nyingine Ethiopia Airline ambayo itabeba tani 19 za minofu ya samaki,” alisema.

Aidha, waziri huyo alisema Jumapili (Mei 24), ndege ya Ethiopia itarudi tena jijini Mwanza na kubeba tani 40 ya minofu ya samaki.

“Tunaendeleza mazungumzo uwanja wa Mwanza umefunguka na kwa kuwa ni uwanja wa kimataifa, ndege zitaruka kimataifa kwa ajili ya kubeba mizigo na tunaendelea kuongea na Waziri wa Mifugo na Uvuvi na nyama ianze kusafirishwa,” alisema.

Katika hatua nyingine, Waziri Kamwelwe alisema Shirika la Ndege (ATCL) linakamilisha taratibu za kuanza kubeba na kupeleka mizigo Ulaya kwa ajili ya biashara.

Aprili, 11, mwaka huu, Mamlaka ya Usafiri wa Anga nchini (TCAA), ilifuta safari zote za ndege za abiria kutokana na mlipuko wa ugonjwa wa corona.

Hata hivyo, kutokana na tathmini ya mwenendo wa ugonjwa huo, Mei 18, mwaka huu, serikali ilitangaza kufunguliwa kwa usafiri wa anga la Tanzania kwa ndege zote za kibiashara, misaada, kidiplomasia, za dharura na ndege maalum.

Habari Kubwa