Watano mbaroni mauaji ya Watanzania Msumbiji

16Jul 2019
Renatus Masuguliko
GEITA
Nipashe
Watano mbaroni mauaji ya Watanzania Msumbiji

JESHI la Polisi nchini limesema watu watano wamekamatwa wakituhumiwa kuhusika na mauaji ya Watanzania tisa Msumbiji mwezi uliopita.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro.

Usiku wa kuamkia Juni 28, mwaka huu, Watanzania tisa waliripotiwa kuuawa kwa kupigwa risasi na wengine sita kujeruhiwa Msumbiji baada ya kuvamiwa wakiwa kwenye mashamba yao ya mpunga na watu waliovalia sare zilizodaiwa kufanana na za Jeshi la Msumbiji.

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP) Simon Sirro, wakati wa uzinduzi wa nyumba 20 za askari polisi mkoani Geita, alimweleza Rais John Magufuli kuwa hakuna damu ya Mtanzania itakayomwagika bure.

IGP Sirro alibainisha kuwa kati ya watuhumiwa watano waliokamatwa, mmoja amefariki dunia na uchunguzi wa kina bado unaendelea.

Alisema Jeshi la Polisi litahakikisha raia wote na mali zao wanalindwa na ndiyo sababu baada ya kupata taarifa za mauaji ya Watanzania Msumbiji, mara moja lilichukua hatua kuwasaka wahusika.

“Hadi sasa, tunawashikilia watuhumiwa watano na mmoja kati yao, ametangulia mbele ya haki... na upelelezi bado unaendelea na wanaendelea kutajana wao kwa wao, hivyo zoezi hilo lipo katika hatua nzuri Mheshimiwa Rais.

"Na imebainika mchezo na mkakati wote wa kupanga njama za mauaji hayo ulifanyika Tanzania," IGP Sirro alisema.

Akizungumzia hatua hiyo, Rais John Magufuli alilipongeza jeshi hilo kwa utendaji wake na kulihakikishia kuwa Watanzania wengi wana imani nalo pamoja na majeshi mengine yalipo nchini.

Akiwa mkoani Geita jana, Rais Magufuli alizindua nyumba 20 kwa ajili ya askari polisi, ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa kujenga nyumba 400 za askari wa jeshi hilo nchi nzima unaofanyika kwa Sh. bilioni 10 alizozitoa kiongozi huyo wa nchi.