Watano mbaroni tuhuma wizi magari

24Jan 2021
Elisante John
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Watano mbaroni tuhuma wizi magari

WATU watano wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani Njombe kwa tuhuma za kuhusika na wizi wa magari saba yaliyokamatwa katika mikoa mbalimbali nchini.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Njombe, Hamisi Issah, aliwaambia waandishi wa habari jana kuwa magari hayo yamekamatwa yakihusishwa na wizi baada ya msako wa kutafuta gari moja lililoibwa maeneo ya Chaugingi mjini  Njombe.

Alisema magari yaliyokamatwa ni aina ya Noah linalodaiwa kuibwa mkoani Mbeya, gari aina ya Spacio lililotoka Silali mkoani Mara, Rav 4 lililokamatwa mkoani Singida na Carina lililopatikana mjini Njombe.

“Tulikuwa tunatafuta gari moja, matokeo yake tumeweza kukamata magari mengine saba ambayo yanahusishwa na kuibwa maeneo mbalimbali katika nchi yetu," alisema Kamanda Issa.

Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Edrick Husein, maarufu Kimyakimya kutoka Dar es Salaam, Sudy Mwinyi, mkazi wa Uyole, Mbeya, Method Mkongwa, mkazi wa Njombe, Imani Fidelis, mkazi wa Moshi na Timothy Nehemia, mkazi wa Mufindi mkoani Iringa.

Kamanda Issa alisema watuhumiwa hao wanadaiwa wanashirikiana kuiba magari na kuyapokea kisha wanayabadilisha namba na hutumia vifaa maalum katika kubadilisha namba za injini.

"Vifaa vyenyewe ukiviangalia vimeandikwa namba kuanzia 0-9, namba ambazo zipo kwenye magari ,hivi huwa vinagongwa kwenye namba endapo ukitaka kubadilisha kwenye injini au kwenye chesesi na bado kuna dawa wanayotumia kufuta namba kwa kusugua," alisema Issah.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakitumia vifaa mbalimbali katika wizi wa magari na kuyabadilisha ili wahusika wa magari hayo washindwe kuyatambua pindi wayaonapo.

Alisema watuhumiwa hao wanaonekana kuwa wazoefu, waliokuwa na mtandao kutoka mikoa mbalimbali ambao umenaswa mkoani Njombe.

Aliwataka wananchi ambao wameibiwa magari za aina hiyo, kwenda kuyatambua akionya kuwa yaliyoingizwa nchini  bila kulipiwa kodi, ni lazima yalipiwe.

"Tutashirikiana na TRA ili kuhakikisha kodi ya serikali inakusanywa, haya magari yalikuwa yanamilikiwa na watu, hivyo kaa mkao wa kujibu gari namna ulivyolipata, ukieleza tofauti utakuwa sehemu ya tukio la wizi," alionya.

Meneja wa Mamlaka ya Mapato (TRA) Mkoa wa Njombe, Shaban Musibu, alisema kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi mpaka sasa magari saba yamekamatwa, hivyo kwa mujibu wa sheria, wamegundua kuna magari kadhaa yameingizwa bila ya utaratibu wa sheria, hivyo wahusika wamekwepa kodi.

Alisema mpaka sasa magari mawili wamiliki wake wamekwepa kodi lakini bado uchunguzi unafanyika ili kubaini kama kuna magari mengine.

Habari Kubwa