Watanzania wawili kurusha Satellite

10Sep 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania wawili kurusha Satellite

WAHITIMU wawili wa Shahada ya Uhandisi wa Umeme na Mawasiliano katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph, wamesafiri kuelekea nchini Italia katika Chuo Kikuu cha Parma kujifunza namna ya kurusha Satellite angani.

Akizungumza katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Prof. Innocent Ngalinda, amesema wahitimu hao wanaenda kuendelea na masomo ya Shahada ya Uzamili.

Amesema wanafunzi hao wanaenda Italia kujifunza namna yakurusha Satellite wakati Tanzania ikijiandaa kufanya hivyo na kwamba hivi karibuni wanafunzi wengine kumi wataelekea India kujifunza masuala hayo kutokana na India kuongoza katika urushaji wa Satellite nyingi duniani.

“Wahitimu hawa wanaenda masomoni Italia ikiwa ni mpango wa ushirikiano wetu na vyuo vya nje ya nchi, katika kuwapeleka wanafunzi kusoma masuala mbalimbali bila gharama yoyote katika kuhakikisha Tanzania inafika katika uchumi wa viwanda kwa vitendo,” Prof. Ngalinda amesema.

Aidha, amewawataka wanafunzi wengine wanaosoma katika chuo hicho, kusoma kwa bidii ili kufika malengo yao kwa wakati sahihi kama walivyofanya wenzao wanaoelekea Italia na India.

Kwa upande wa Penina Mbwilo ambaye ni mmoja wa wahitimu wa Shahada ya Uhandisi wa Umeme na Mawasiliano katika chuo hicho, amesema ilikuwa ni ndoto kwake kumaliza masomo ya shahada nakuendelea na masomo ya juu zaidi.

“Malengo yangu ni kupata ujuzi zaidi na kuwasaidia wengine katika ujuzi huo kwa kuwafundisha ili na wao kupata nafasi kama aliyopata mimi,” Mbwilo amesema.

Habari Kubwa