Watanzania 22 jela kwa kuzamia 'Sauzi'

25Jan 2020
Hellen Mwango
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania 22 jela kwa kuzamia 'Sauzi'

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar es Salaam, imewahukumu Watanzania 22 waliozamia isivyo halali Afrika Kusini, kwenda jela kutumikia kifungo cha miezi sita baada ya kukiri kutoka nchini bila kufuata taratibu.

Washtakiwa hao ni pamoja na Mzuzuri Mohammed, Mohammed Said, Masoro Musa, Mneke Mehra, Kibila Husein, Ali Hassan, Jamalino Rashid, Abdul Nassoro, Waziru Adam na Said Salum.

Wengine ni, Chuwa Sadick, Salum Kasimum, Macalot Alex, Kayenga Winston, Idali Charles, Ibrahim Mohammed, Jafari Zebra, Omane Fizo, Mbona Edson, Ulembo Azide, Fizo Charles na Mnangwa Rajab.

Hukumu hiyo ilitolewa jana na Hakimu Mkazi, Vick Mwaikambo aliyesikiliza kesi hiyo.

Alisema mahakama yake inawaona washtakiwa wote ni vijana, nguvu kazi ya Taifa la Tanzania, lakini wameondoka nchini na kuzamia Afrika ya Kusini bila kufuata sheria za Idara ya Uhamiaji.

"Mahakama hii inawatia hatiani kwa kuondoka nchini bila kufuata sheria za Idara ya Uhamiaji, mtakwenda jela kutumikia kifungo cha miezi sita, mmeliingizia gharama taifa kwa kukodi ndege ya kuwarudisha nchini wakati fedha hizo zingeweza kujenga hospitali na kufanya shughuli nyingine za maendeleo," alisema.

Hakimu alisema washtakiwa watakwenda jela kutumikia adhabu hiyo pamoja na kufanya kazi mbalimbali watakazopangiwa na magereza.

Kabla ya kutolewa kwa adhabu hiyo, Wakili wa Serikali, Shija Sitta, aliiomba mahakama kutoa adhabu kali kwa washtakiwa ili iwe fundisho kwa vijana wengine.

Alidai taratibu za kusafiri nje ya nchi zipo na kwamba hakuna msingi wa watu kwenda Afrika Kusini bila kibali, kitendo ambacho kimedhalilisha taifa kwa kuonekana ni wahamiaji haramu.

Washtakiwa hao kwa nyakati tofauti waliiomba mahakama iwapunguzie adhabu ili kulitumikia taifa.

Awali, akisoma mashtaka, Sitta alidai washtakiwa hao walitoka nje ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kinyume cha Kanuni za Uhamiaji namba 20(3)(a) G.N namba 657 ya mwaka 1997 inayosomwa pamoja na kifungu namba 48(2) cha Sheria ya Uhamiaji namba 54 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2016.

Alidai Januari 21, mwaka huu, maeneo ya Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA), washtakiwa hao, wakiwa raia wa Tanzania, walikutwa wakiwa wametoka nje ya nchi bila kufuata utaratibu wa kutoka nchini kwenda Afrika Kusini kwa kupitia mipaka inayojulikana.

Washtakiwa wote walikubali mashtaka hayo na upande wa mashitaka uliwasomea maelezo ya awali ambapo alidai tarehe zisizofahamika, walitoka Tanzania na kuingia Afrika Kusini bila kufuata taratibu.

Ngwijo alidai katika tarehe hiyo, washtakiwa walikamatwa Afrika Kusini na kuletwa Tanzania na kwamba walifikishwa kwenye Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere na kupelekwa Ofisi ya Mkoa wa Dar es Salaam na kuchukuliwa maelezo.

Hata hivyo, washtakiwa wengine 20 walifikishwa mahakamani hapo, lakini hawakusomewa mashtaka kutokana na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Agustina Mbando aliyepangiwa kesi hiyo, kupata dharura hivyo kesi hiyo iliahirishwa hadi Jumatatu (Januari 27, mwaka huu).

Habari Kubwa