Watanzania waaswa kuangalia maendeleo ya Magufuli miaka mitano

09Aug 2020
Mary Geofrey
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watanzania waaswa kuangalia maendeleo ya Magufuli miaka mitano

WATANZANIA wametakiwa kuangalia mambo makubwa ya kimaendeleo yaliyofanywa chini ya usimamizi wa Rais John Magufuli ndani ya miaka mitano badala ya kusikiliza kelele za wanasiasa wasiyolitakia mema Taifa.

RAIS JOHN MAGUFULI.

Hayo yameelezwa leo na Mwanaharakati, Habibu Mchange,  jijini Dar es Dar es Salaam wakati akitolea ufafanuzi kauli za wanasiasa wanaowania urais wakibeza juhudi za Serikali chini ya Rais Magufuli.

Alitolea mfano ujenzi wa Bwawa la Nyerere (Stieglers Gorge) katika Mto Rufiji litakalozalisha Megawati 2115 za umeme nchi nzima.

Amesema si kweli kuwa kabla ya kuanza ujenzi wa bwawa hilo hakukuwa na vyanzo vingine vya kuzalisha umeme, lakini kukamilika kwa bwawa hilo kutazalisha umeme mara mbili ya unaozalishwa sasa na vyanzo vyote vya uzalishaji.

“Kumsifia Rais Magufuli kwa jambo hilo ni makosa,” alihoji Mchange na kuongeza: “Wakati Rais Magufuli akiingia madarakani mwaka 2015 alikuta Tanzania ina ndege moja, lakini kabla ya hapo hatukatai kusema Tanzania ilikuwa na ndege nyingi zaidi ya 10 lakini hazikuwepo kwa namna fulani fulani ikiwamo kuharibika, lakini ndani ya miaka mitano amenunua ndege 11, nalo hilo kumpongeza ni makosa?”

Amesema Serikali imefanikiwa kupunguza deni la Taifa na kwamba taarifa zinazozungumka mitandaoni hazina ukweli.

“Oktoba mwaka 2015 deni la taifa lilikuwa Sh. trilioni 26.8 kwa Serikali na sekta binafsi lilikuwa Sh. trilioni 6.5, jumla Sh. trilioni 31. 

Hadi Aprili 2020, deni limefikia Sh. trilioni 40, ukitoa na deni la awali maana yake ndani ya miaka mitano Serikali na sekta binafsi wamekopa jumla ya Sh. trilioni 13,” amesema Mchange.

Amefafanua zaidi kuwa , "Wanasiasa wasiwachanganye Watanzania bali wawaeleze ukweli ulivyo bila kuongeza chumvi kwa kuwa watu wameamka sasa si kama zamani, ukisema uongo unachukua siku kadhaa kupata majibu. Ndio maana tumeamua sisi hatutaki Rais Magufuli awajibu hawa wababaishaji sisi tumejitolea kumjibia.”

Amesisitiza, hata katika mfumo wa kubadilisha fedha za kigeni kadiri shilingi ya Tanzania inapopanda na kushuka dhidi ya Dola ya Kimarekani, deni la taifa pia linapanda na kushuka.

Habari Kubwa