Watanzania waondolewa hofu corona

17Feb 2020
Woinde Shizza
Arusha
Nipashe
Watanzania waondolewa hofu corona

Dk. Ndugulile alitoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari akiwa jijini Arusha katika ziara zake za kikazi.

Katika maswali yao waandishi walitaka kujua kuhusu tetesi za kuwapo kwa ugonjwa huo nchini, pamoja na kufahamu ukweli wa taarifa za mtu anayedai kuwa na dawa za ugonjwa huo.

NAIBU Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, picha mtandao

Dk. Ndugulile alitoa kauli hiyo kwa waandishi wa habari akiwa jijini Arusha katika ziara zake za kikazi.

Katika maswali yao waandishi walitaka kujua kuhusu tetesi za kuwapo kwa ugonjwa huo nchini, pamoja na kufahamu ukweli wa taarifa za mtu anayedai kuwa na dawa za ugonjwa huo.

“Niseme tu kuwa Tanzania mpaka sasa hivi bado tuko salama na hakuna mgonjwa yeyote ambaye ameripotiwa na amethibitika kuwa na ugonjwa,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema serikali inafuatilia taarifa mbalimbali za washukiwa na watu wote ambao wanawahisi kuwa na ugonjwa huo na kuwapima na kubaini kuwa hawana ugonjwa.

“Tumeendelea kuchukua tahadhari mbalimbali na mimi niko katika mkoa huu wa Arusha na nitaenda Kilimanjaro kwenda kuangalia utayari,” alisema Dk. Ndugulile na kuongeza kuwa ameridhika na maandalizi ya mkoa huo katika kudhibiti ugonjwa huo.

Akijibu kuhusu mtu aliyedai kuwa na dawa ya kutibu ugonjwa huo ambaye anajulikana kwa jina la Mosses Mollel, maarufu kwa jina la ‘Nabii namba saba’, Dk. Ndugulile alisema ana taarifa za mtu huyo ambazo zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii na vyombo vya habari akijitangaza kuwa anayodawa ya kutibu ugonjwa huo na kumtaka athibitishe kauli yake.

“Kimsingi nimeiona hiyo taarifa ya huyo mtu anayejiita Nabii Saba kuwa anayo dawa ya kutibu ugonjwa wa corona, ila hapa kwetu Tanzania hatuna maambukizi yoyote ya ugonjwa huyo, tunachotaka huyo mtu atuthibitishie uwezo wake wa kutibu huo ugonjwa wa corona,” alisema Ndugulile.

Alisema kama atashindwa kuthibitisha atachukuliwa hatua kali za kisheria.

Dk. Ndugulile alisema serikali imetuma wataalamu wake kwenda kumsaka na kumhoji kama ana vibali vya kutoa huduma ya tiba na kujitangaza kuwa anatoa huduma ya kutibu ugonjwa huo hatari ambao hadi sasa mataifa bado yanahaha kusaka tiba.

Mollel mkazi wa Ngaramtoni wilayani Arumeru, amekuwa akijitangaza kuwa ana dawa ya kutibu ugonjwa huo wa virusi vya corona na kuweka mawasiliano yake kwenye mitandao.

Dk. Ndugulile alitahadharisha kuwa mtu yeyote anayetoa tiba asili na mbadala lazima asajiliwe na mamlaka husika ambayo ni Wizara ya Afya, lazima dawa zake ziwe zimesajiliwa na Wizara ya Afya na kusisitiza kuwa nabii huyo pia anapaswa kuthibitisha amesajiliwa wapi na lini.

“Tuepuke kutoa kauli ambazo zinakwenda kuchanganya jamii, na endapo tutabaini mtu huyu hana sifa ambazo anasema kuwa nazo tutamchukulia hatua za kisheria,” alisema.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Arusha, Jonathan Shana, alisema kuwa jeshi hilo lilimkamata na kumpeleka kwa Mganga Mkuu kwa ajili ya kumuhoji kama kweli ana dawa hizo.

"Sisi tulimkamata na kumpeleka kwa Mganga Mkuu ili amuhoji na kumwangalia kama ana vibali vya kugawa hiyo dawa na nifafanue sisi tulimchukua na kumpeleka kwa Mganga Mkuu hatumshikilii,” alisema Shanna.

Habari Kubwa