Watanzania watakiwa kujitokeza kuchangia damu salama

16Jan 2020
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania watakiwa kujitokeza kuchangia damu salama

WATANZANIA wametakiwa kujitokeza kuchangia damu wakati wowote badala ya kusubiri majanga yatokee, kwa ajili ya kusaidia makundi ya watu wanaohitaji huduma hiyo kwa wingi ambao ni majeruhi wa ajali, wajawazito, watoto na wagonjwa wa saratani.

Rai hiyo ilitolewa jana na Meneja wa Mpango wa Taifa wa Damu Salama, Dk. Magdalena Lyimo, wakati akizungumza na maofisa mawasiliano wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wakati wa ziara ya kampeni ya 'Tumeboresha Sekta ya Afya' kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais John Magufuli.

Alisema Watanzania wengi wanapenda kujitokeza kuchangia damu wakati yanapotokea majanga mbalimbali kama ajali za barabarani na moto.

Alitolea mfano wa tukio la ajali ya moto ililotokea eneo la Msavu mkoani Morogoro Agosti 10, mwaka jana
na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 100, katika kipindi cha muda mfupi walikusanya chupa 2,328 za damu kutoka mikoa mbalimbali nchini.

"Wito wetu kwa jamii ni kuendelea kujitokeza kuchangia damu kwa wingi kwa ajili ha kusaidia wenzetu wanaopata majanga ya ajali ili kuokoa maisha yao.

Kwa kipindi ilipotokea ajali ya lori la mafuta mkoani Morogoro mwaka jana, jumla ya watu 2,328 waliojitokeza kuchangia damu kwa ajili tu ya kusaidia majeruhi kutoka maeneo mbalimbali nchini," alisema Dk. Lyimo.

Alisema kwa kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Magufuli, wamefanikiwa kuongeza ukusanyaji wa damu kutoka asilimia 40 mwaka 2016/17 hadi asilimia 60 mwaka 2018/19.

Alisema kwa mwaka wanakusanya chupa za damu 390,379 kwa takwimu za mwaka 2018/19 kutoka chupa 257,557 mwaka 2017/18  wakati lengo likiwa ni kukusanya chupa 500,000 kwa mwaka sawa na asilimia 100 ya mahitaji yote.

Alisema kwa mwezi wanakusanya damu kutoka kwenye vituo vyao vilivyopo kote nchini chupa 25,000 hadi 30,000.

Kadhalika alisema wameboresha utendaji kazi kutokana na Serikali kununua mashine za kisasa za upimaji mpya 24 zilizosambazwa katika kanda sita za ofisi zao.

Alisema mashine hizo zilizonunuliwa kwa gharama ya Sh. bilioni 13.248 na zina uwezo wa kupima Homa ya Ini B na C, Kaswende na Maambukizi ya Ukimwi kwa wakati mmoja.

Habari Kubwa