Watanzania watakiwa kumwenzi Nyerere kwa kudumisha amani

15Oct 2020
Sabato Kasika
Dar es Salaam
Nipashe
Watanzania watakiwa kumwenzi Nyerere kwa kudumisha amani

WATANZANIA wametakiwa kulinda amani, umoja na mshikamano vilivyopo ili waendelee kufanya shughuli zao kwa uhuru bila vurugu na kujiletea maendeleo, kwa manufaa ya vizazi vilivyopo na vijavyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Utawala Bora na Maendeleo Tanzania (CEGODETA), Thomas Ngawaiya, alisema hayo jana wakati akitoa salamu za taasisi hiyo kuhusu kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere.

Alisema kumbukumbu ya miaka 21 ya kifo cha Baba wa Taifa, imekuja wakati zimebakia wiki chache Watanzania washiriki katika uchaguzi mkuu.

"Sisi kama watu tunaohimiza utawala bora, hatunabudi kuendelea kuwakumbusha Watanzania kulinda, amani umoja na mshikamano kwa ajili ya vizazi vilivyopo na vijavyo," alisema Ngawaiya.

Alisema kuvunja amani ni rahisi, lakini kuirudisha ni vigumu, hivyo ili kumuenzi Baba wa taifa, kila Mtanzania anatakiwa kuwa mtu wa kuhimiza mwenzake kulinda amani iliopo nchini.

"Niwakumbushe tu kwamba, Baba wa Taifa alianza kazi ya kupigania amani na hata alipong'atuka aliendelea kuhimiza amani, hivyo amani iwe ni wimbo wa kila mmoja na hasa wanasiasa," alisema.

Alisema, wakati wa kampeni, wanasiasa wawe makini na kuepuka kutukana wenzao ama kutumia maneno ya kuudhi badala yake watangaze sera na ilani za vyama vyao kwa wananchi.

"Kama watu wanakupenda watakuchagua tu bila hata kutukana ama kutumia lugha ya kuudhi dhidi ya wagombea wengine, kwani kufanya hivyo kunaweza kuamsha hasira za watu na kusababisha amani ivurugike," alisema Ngawaiya.

Aliongeza kuwa, Watanzania ni watu wa amani, hivyo wasiingizwe katika mambo ambayo hawakuyazoea, na kwamba hawana ujasiri wa kupigana kama walivyo baadhi ya wengine ambao nchi zao hazina amani.

Habari Kubwa