Watatu mbaroni kujihusisha na unyang’anyi kwa kutumia silaha

18Jan 2022
Na Mwandishi Wetu
Mbeya
Nipashe
Watatu mbaroni kujihusisha na unyang’anyi kwa kutumia silaha

JESHI la Polisi mkoani Mbeya linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kujihusisha na  matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha.

Taarifa hiyo imetolewa leo Januari 18, 2022 na Kaimu Kamanda wa Polisi mkoani Mbeya, ACP Christina Musyani,ambapo pia amewataja watumiwa hao kuwa ni Msafiri  (46) mkazi wa Usangu Wilaya ya Mbarali, Boniface Shupa (36) mkazi wa Matundasi pamoja na Onesmo Bolisi Mwachawi (38) Mkazi wa Makongolosi.

Taarifa hiyo imeeleza kuwa watuhumiwa hao walikamatwa Januari 15, mwaka huu majira ya saa 5:45 usiku huko katika Mji Mdogo wa Makongolosi wilayani Chunya katika misako inayoendeshwa na Jeshi la Polisi dhidi ya wahalifu wa matukio mbalimbali.

Katika upekuzi uliofanywa na Jeshi hilo watuhumiwa walikutwa na bunduki mbili bastola moja na Gobole moja zilizotengenezwa kienyeji, risasi 10 za shot gun, simu za mkononi tatu, tochi moja, panga moja, kofia mbili na mizula miwili ambavyo hutumia katika matukio ya uhalifu.

Imeeleza kuwa watuhumiwa wamehojiwa na kukiri kuhusika kwenye matukio mawili ya unyang’anyi wa kutumia silaha likiwemo tukio la Januari 2, 20211 majira ya saa 3:30 usiku huko matundasi ambapo walivamia duka la Andreas John (22) na kumpora fedha taslimu shilingi 1,100,000/- pamoja na vitu mbalimbali vyenye thamani ya shilingi 5,490,000/- na kumjeruhi mke wa mhanga aitwaye Sarah Frank (21) Mkazi wa Matondo.

Pia mnamo tarehe 14.01.2022 majira ya saa 2:00 usiku walivamia duka moja huko katika eneo la Mnazi Mmoja Chunya na kupora fedha taslimu shilingi 1,925,000/-, simu za mkononi na vitu mbalimbali. Upelelezi wa shauri hili unaendelea na mara baada ya kukamilika watuhumiwa watafikishwa mahakamani.

Habari Kubwa