Watatu mbaroni tuhuma za kukutwa na nyara za serikali, bangi

24Sep 2021
Julieth Mkireri
Rufiji
Nipashe
Watatu mbaroni tuhuma za kukutwa na nyara za serikali, bangi

​​​​​​​WATU watatu wanashikiliwa na Jeshi la Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji kwa tuhuma mbali mbali ikiwemo ya mwanamke (21) kukutwa na nyara za Serikali.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Kipolisi Rufiji Protas Mutayoba akionyensha nyara Ilizokamatwa.

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Rufiji Protas Mutayoba, amesema tukio la kukutwa na nyara limetokea  Septemba 22 majira ya saa moja usiku maeneo ya Utunge-Kisemvule wilayani Mkuranga ambapo watu wawili walikamatwa.

Amesema watuhumiwa hao ambao majina yao yamehifadhiwa ni mwanaume (40) na mwanamke (21) wakiwa na nyara za serikali zidhaniwazo kuwa ni meno ya tembo vipande 16 vyenye uzito wa kilo 25.

Aidha, Kamanda Mutayoba amesema watuhumiwa hao wanashikiliwa na Jeshi hilo kwa uchunguzi zaidi na hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yao.

Katika tukio lingine Kamanda Mutayoba amesema Septemba 16 majira ya usiku huko kitongoji cha Matope-Kimanzichana Wilaya ya Mkuranga Jeshi la Polisi lilimkamata mtuhumiwa mmoja mwanaume (43) akiwa na kilo 150 za bangi

Kamanda Mutayoba amesema mtuhumiwa huyo ameshafikishwa mahakamani kwa kosa la kupatikana na bangi.