Watatu Uhamiaji wasimamishwa kwa kutumia nguvu kumdhibiti mtuhumiwa

30May 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es salaam
Nipashe Jumapili
Watatu Uhamiaji wasimamishwa kwa kutumia nguvu kumdhibiti mtuhumiwa

WIZARA ya Mambo ya Ndani ya Nchi Idara ya Uhamiaji, imewasimamisha kazi wafanyakazi watatu kutokana na tukio la Askari wa Uhamiaji kutumia nguvu dhidi ya Alex Raphael Kyai kama video fupi iliyosambaa katika mitandao ya kijamii.

Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala.

Akizungumza na wandishi wa habari leo Mei 30, 2021 Kamishina Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala, amesema mnamo Mei 27 mwaka 2021, Idara ya Uhamiaji ilimkamata mtuhumiwa wa utapeli anayefahamika kwa jina Alex Raphael Kyai katika Ofisi ya Uhamiaji Kurasini mkoani Dar es salaam ambaye aliongozana na mteja wa huduma za pasipoti, aliyemtambulisha kama mkewe.

Aidha Dk. Makakala amesema baada ya mahojiano, ilibainika kuwa mtuhumiwa huyo amekuwa na tabia ya kuwalaghai na kupokea fedha kutoka kwa wateja mbalimbali ili waweze kupata pasipoti kwa haraka, pia mtuhumiwa huyo amekuwa akijitambulisha kama Mtumishi wa Taasisi nyeti ikiwemo Taasisi ya Kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

"Idara ya Uhamiaji inakiri kutokea kwa tukio hilo na pia inalaani kitendo kilichofanywa na askari wa Uhamiaji kwa kutumia nguvu kinyume cha sheria na maadili ya kazi zao, hata hivyo Idara ya Uhamiaji tayari imechukua hatua za kinidhamu dhidi ya askari hao" amesema Dk. Makakala.

Sambamba na hayo, Idara ya uhamiaji inatoa wito kwa Wananchi wote wanaohitaji huduma za kiuhamiaji kufika wenyewe katika ofisi za Uhamiaji, pia Uhamiaji wanawahakikishia kwamba idara itaendelea kutoa huduma zake kwa weledi, uwazi na bila kutumia mtu wa kati ( Vishoka).

Aidha Idara ya uhamiaji imetoa onyo kwa yeyote ambaye atajaribu kujifanya kuwa Afisa wa Uhamiaji au Afisa wa Serikali ili kumsaidia mtu mwingine kwa maslahi yake binafsi hatua kali dhidi yake zitachukuliwa kwa mujibu wa Sheria, Pia idara hiyo imewataka Watanzania wote kutoa ushirikiano katika kutoa taarifa za watu wanaofanya vitendo vya aina hiyo.

Habari Kubwa