Wateja watelekeza mabilioni benki zilizofilisiwa

26Feb 2021
Salome Kitomari
Mtwara
Nipashe
Wateja watelekeza mabilioni benki zilizofilisiwa

BODI ya Bima ya Amana imesema wateja 38,654 kati ya 63,704 wa zilizokuwa benki saba ambazo zimefungiwa, hawajajitokeza kuchukua fedha zao ambazo wanapaswa kulipwa kwa mujibu wa sheria.

Aidha, wateja 25,050 ambao ni sawa na asilimia 39, walijitokeza kuchukua fedha hizo na wateja hao ni wale waliokuwa na viwango vikubwa na kwamba kati ya Sh. bilioni 11 zimechukuliwa Sh. bilioni 7.3.
 
Hayo yalisemwa jana na Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima ya Amana, Richard Malisa, wakati akiwasilisha mada ya bodi hiyo, mafanikio na changamoto.
 
Alizitaja Benki hizo kuwa ni Covenant Bank for Women (T) Limited, Efatha Bank Limited, Kagera Farmers Cooperative Bank, Mbinga Community Bank Limited, Meru Community Bank Limited, Njombe Community Bank Limited na FBME Bank Limited.
 
“Baadhi hawajaja kwa kuwa kiwango ni kidogo ikilinganishwa na maeneo wanayotoka na wengine taarifa hazijawafikia kuwa benki ikifungwa kuna utaratibu wa kupata fidia, tunawaomba kokote waliko waje kuchukua fedha zao,” alisema.

“Tunawaomba wateja hawa watambue kuwa inapofungwa benki, serikali kwa mujibu wa sheria, imeweka utaratibu watu watapewa fidia na kwa utaratibu watu zaidi ya asilimia 90 wanakuwa hawajapoteza chochote. Kiwango cha Sh. milioni 1.5 ni baada ya kufanya uchambuzi wa waliokuwa na amana,” alifafanua.
 
Alisema kiwango kinacholipwa ni kuanzia Sh. moja hadi milioni 1.5 na kama amana amezibakiza, atasubiri utaratibu wa kufilisi mali na kukusanya madeni ya benki husika.
 
Malisa alisema walianza na Sh. 250,000 mwaka 1994 na mwaka 2003 wakafika 500,000 kisha baadaye Sh. milioni 1.5 ambayo hulipwa kwa idadi ya amana na si idadi ya akaunti alizokuwa nazo mteja na kinachofanyika zinakusanywa kwa pamoja.
 
“Tunaposema asilimia 90 hawatapoteza chochote ni wale ambao wana kiwango cha chini ya Sh. mil 1.5 wanalipwa chote isipokuwa walio na zaidi ya kiwango hicho,” alisema.
 
Alisema wenye fedha nyingi watasubiri ufilisi ambao hufanywa na mfilisi ambaye ana wajibu wa kuuza mali na kukusanya madeni na kuuza ili kinachopatikana kigawanywe kwa waliokuwa wanaidai benki kwa kiwango kinachozidi Sh. milioni 1.5.
 
Malisa alisema kwa sasa kinachofanyika ni kuuza madeni na kuuza mali za benki hizo, ili fedha zipatikane na kuwalipa wateja.
 

Habari Kubwa