Watendaji wazuiwa kutumia nguvu msako mifuko plastiki

22May 2019
Mary Geofrey
DAR
Nipashe
Watendaji wazuiwa kutumia nguvu msako mifuko plastiki

SERIKALI imewataka watendaji na watumishi wa mkoa wa Dar es Salaam, kutotumia nguvu kuwapigana virungu wananchi watakaokutwa na mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, January Makamba, akizungumza na viongozi na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam jana, kuhusu kupiga marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini. PICHA: GETRUDE MPEZYA

Aidha, amepiga marufuku watendaji watakaosimamia kazi hiyo kutoingia kwenye maduka, ofisi na kwenye magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.

 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, (Muungano na Mazingira), January Makamba, alitoa angalizo hilo jana, wakati akizungumza na watendaji wa mkoa wa Dar es Salaam, wakiwamo wakuu wa wilaya, makatibu tawala, wakurugenzi, madiwani, wenyeviti na watendaji wa kata na mitaa, wasimamizi wa masoko, maofisa afya, mazingira na biashara kujadili utekelezaji wa marufuku ya mifuko ya plastiki.

 

“Katika utekelezaji wa sheria hii mpya inayoanza Juni Mosi, mwaka huu, hatutegemei kuona watu wanaendelea kubeba mifuko, lakini pia hatutegemei kuona kinamama wanapigwa virungu na mgambo kisa wamebeba mifuko na wala hatutegemei kuona watu kuporwa mali zao,” alisema Makamba.

Alieleza katika utekelezaji wa sheria hiyo, watendaji watakaosimamia kazi hiyo hawapaswi kuingia kwenye ofisi, maduka na kufungua magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko ya plastiki.

“Tunatarajia hakuna mwananchi ambaye atatumia mifuko ya plastiki kuanzia Juni Mosi, lakini watendaji wanaosimamia kazi hii, hatutarajii kuona wanapita kwenye ofisi, maduka na kufungua magari ya watu kutafuta mizigo ya mifuko hili hatulitarajii kabisa,” alisema Makamba.

Alisema katika utekelezaji wa jambo hilo, mwananchi ambaye atakutwa amebeba au mfanyabiashara anayeuza mifuko ya plastiki ndiye atawajibishwa kwa mujibu wa sheria.

Kadhalika, alisema mpango huo unaenda sambamba na kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu udhibiti wa matumizi ya mifuko hiyo.

“Tutatumia muda mrefu kuendelea kuelimishana na kuelekezana kuhusu kuacha matumizi ya mifuko hii ya plastiki, hivyo utekelezaji wake hatutegemei ukitumika kuwanyanyasa watu na kupora mali zao,” alisema Makamba.

Makamba alisema pia faini zitakazotozwa kwa wananchi watakaokutwa wamekiuka sheria hiyo, zitatumika katika halmashauri husika hadi hapo wizara itakapotoa mwongozo mwingine.

Alishauri maofisa mazingira kwenye mitaa husika kuwa wasimamizi wa kazi hiyo badala ya kila mtendaji kuwa mtekelezaji jambo ambalo alisema litaleta usumbufu kwa jamii.

Kwa upande wake, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa-Tamisemi), Mwita Waitara, alisema utekelezaji wa agizo hilo utaenda sambamba na utoaji wa elimu zaidi kwa jamii.

Alisema utekelezaji wa sheria hiyo hautahusika kutumia nguvu ya vyombo vya dola isipokuwa watafanya hivyo endapo ikibidi.

Naye Mwanasheria Mkuu wa Baraza la Usimamizi na Uhifadhi wa Mazingira (Nemc), Heche Suguta, alisema utekelezaji wa sheria hiyo si kwa ajili ya kuwaonea wananchi bali kusaidia kudhibiti uharibifu wa mazingira nchini.

Hata hivyo, alisema siyo mifuko yote ya plastiki itakayozuiliwa matumizi yake, bali kuna baadhi ya vifungashio vya plastiki vitaendelea kutumika kama vile vya dawa za binadamu, pembejeo za kilimo, vya kiwandani, vya ujenzi na vya maziwa.

Hivi karibuni serikali ilipiga marufuku uzalishaji, uingizaji, usafirishaji nje ya nchi, usambazaji, uuzaji na matumizi ya mifuko aina ya plastiki, maarufu kama ‘rambo’, inayotumika kubebea bidhaa.

Katazo hilo lililotangazwa bungeni jijini Dodoma Aprili 9, mwaka huu na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, tayari limeanza kutekelezwa na ifikapo Juni mosi, 2019 ni mwisho wa matumizi yote ya mifuko hiyo.

Habari Kubwa