WaterAid yasaidia shule mapambano kipindupindu

16Oct 2020
Beatrice Shayo
Kisarawe
Nipashe
WaterAid yasaidia shule mapambano kipindupindu

SHIRIKA lisilo la kiserikali la WaterAid Tanzania, limetoa msaada wa mashine za kunawia mikono kwa wanafunzi zenye thamani ya Sh. milioni 19 ili kujikinga na magonjwa ya milipuko kikiwamo kipindupindu.

Wanafunzi wakinawa mikono kwenye kifaa kilichotengenezewa na Shirika lisilo la kiserikali la WaterAid, na kutolewa msaada kwa shule mbili za msingi ya Chanzige A na Chanzige B, wilayani Kisarawe, mkoani Pwani jaan, ikiwa ni Siku ya Maadhimisho ya Unawaji Mikono Duniani. PICHA: BEATRICE SHAYO

Msaada huo umetolewa kwa shule mbili za msingi ya Chanzige A na Chanzige B zilizoko Wilaya ya Kisarawe, ikiwa ni maadhimisho ya Siku ya Unawaji Mikono Duniani.
 
Akizungumza katika maadhimisho hayo jana, Mkurugenzi Mkazi wa WaterAid, Anna Mzinga, alisema wanatambua umuhimu wa siku ya kunawa mkono na kuamua kuadhimisha pamoja na wanafunzi wa shule hizo kwa kuwapatia msaada.
 
"Tumetoa hivi vifaa vya kunawa mkono pamoja na elimu tuliyowapatia bado kuna haja ya kuwafundisha watoto wetu umuhimu wa kunawa na maji tiririka kwani ni kinga ya kuambukiza magonjwa ikiwamo kipindupindu," alisema.
 
Alisema hata ugonjwa wa corona walifanikiwa kupambana nao kutokana na unawaji wa mkono, hivyo wanaunga na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto katika unawaji wa mkono itasaidia kuwapo na afya salama.
 
"Kampeni hii inalenga uboreshaji wa huduma za maji na usafi wa mazingira ikiwapo na msisitizo mkubwa katika ubadilishaji wa tabia kwa jamii na kuzipokea tabia zinazoshauriwa na wataalam ikiwemo unawaji wa mikono kwa maji na sabuni," alisema.
 
Mzinga alisema pasipo huduma sahihi za maji na usafi wa mazingira katika makazi yetu, shule, vituo vya kutolea huduma za afya na taasisi zingine, mazingira yatakuwa vyanzo vya magonjwa na kuacha jamii ikiwa katika hatari ya kupata milipuko ya magonjwa ya kuambukiza. 
 
Alisema Siku ya Unawaji Mikono Duniani ilianzishwa kwa lengo la kuongeza ufahamu kwa jamii juu ya umuhimu wa kunawa mikono kwa maji na sabuni. Kaulimbiu ya mwaka huu kidunia inasema ‘Usafi wa Mikono kwa Wote’ ikiwa ni wito kwa watu wote kufanya suala la usafi wa mikono liwe ni tabia ya kawaida na ya kudumu.
 
Naye Katibu Twala wa Wilaya ya Kisarawe, Mwanana Uwesu, alisema elimu hiyo itawasaidia wanafunzi hao kujikinga na maradhi mbalimbali na kuwa na afya bora pamoja na kuhudhuria shuleni kwa wingi.
 
Aliwataka wananchi kuweka vifaa vya kunawa mikono katika maeneo yao ili kujikinga na magonjwa.
 
Kaimu Ofisa Elimu Msingi, Salehe Segumba, alishukuru kwa msaada waliopatiwa na kwamba itawasaidia wanafunzi kujiepusha na magonjwa yatokanayo na uchafu.
 

Habari Kubwa