Watetezi wa haki za binadamu watakiwa kuzingatia haki za msingi

07Dec 2021
Beatrice Shayo
Dar es Salaam
Nipashe
Watetezi wa haki za binadamu watakiwa kuzingatia haki za msingi

Askofu Mkuu wa kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dk. Askofu Fredrick Shoo, amewataka watetezi wa haki za binadamu kuzingatia haki za msingi za kila mwanadamu.

Askofu Shoo ameyasema hayo jana wakati akifungua mafunzo ya uongezaji uwezo kwa viongozi wa dini ili kushiriki kutatua changamoto za kijamii hasa kwenye ulinzi na utetezi wa haki za binadamu nchini.

Mafunzo hayo yameandaliwa Kamati ya Viongozi wa Dini inayohusu Haki za Kijamii na Uadilifu wa Uumbaji (ISCEJIC) inayoundwa na Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (BAKWATA) na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT) kwa kushirikiana na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC).

Askofu Shoo amesema kuna kipindi kutaja suala la haki ilikuwa ni jambo gumu, lakini anawaomba watetezi wa haki akiwemo yeye kuzingatia haki za msingi za kila mwanadamu.

"Ni kama ibilisi amefunga midomo ya watanzania tusitaje neno haki, tunataja upendo na Amani peke yake lakini tunahitaji kuongeza haki kwa sababu haki, ni jambo la msingi, pasipo haki hakuna Amani, Amani ni Tunda la Haki” amesema Askofu Shoo.

Hata hivyo, Askofu Shoo amepongeza hatua ya viongozi hao wa dini kuona umuhimu wa kukutana na kujadiliana namna wanaweza kushiriki katika utetezi wa haki za binadamu katika nafasi walizonazo kwenye jamii na kanisa.

“Viongozi wa dini ni wadau wakubwa wa maendeleo katika nchi yetu, kupitia taasisi zetu tunaendesha sehemu kubwa ya utoaji wa huduma za jamii hapa nchini, hii sio siri sisi ni wadau wakubwa maendeleo ya nchi hii.

"Taasisi za dini ni walezi wa jamii kupitia Imani na mafundisho ya imani ambayo msingi wake ni ulinzi na uendelezaji wa utu wa mtu.” amesema Askofu Shoo

Kwa Upande wake Sheikh wa Mkoa wa Kilimanjaro, Sheikh Shaban Mlewa naye amepongeza jitahada hizo zilizochukuliwa na viongozi wa dini katika kujifunza namna mbali mbali za kushiriki katika utetezi wa haki za binadamu.

“Ni vyema tukajua wajibu wetu wa sasa ni kuijenga jamii na kuikumbusha kuzingatia haki, ni wajibu wa kila kiongozi kuwa na huruma, kuwa na imani thabiti, kuonyesha upendo na haki yenyewe ambayo ndio msingi wa yote hayo.

"Kusema kunaweza kusikilizwa na yoyote, lakini utendaji unaweza ukafuatiliwa na wengi, tunaweza kusema lakini tukafuatiliwa tunatenda kama tunavyoamrisha?, mara nyingi tuhamasishe tunayotenda ikiwemo kutenda haki ambayo ni wajibu wetu,” amesema Sheikh Mlewa.

Naye Mtoa mada katika mkutano huo ambaye ni Mratibu kitaifa, THRDC, Onesmo Olengurumwa, amesema anapongeza hatua ya viongozi wa dini kuona umuhimu wa kujadiliana na kuongeza ujuzi katika uzingatiaji wa masuala ya haki ambayo ni msingi wa amani na upendo kwa jamii.

“Dini na maswala ya haki za binadamu ni sawa na pande mbili za shilingi, haviwezi kuachana, ni vitu ambavyo vinakwenda pamoja ni vitu ambavyo vikikaa vizuri na kuelewana vizuri tunaamini tutakuwa na jamii ambayo inaheshimu na kulinda haki za binadamu , na ndio maana leo tumekuja kuwakumbusha kuwa wao ni walinzi namba moja wa haki za binadamu kwa sababu ndio wanaohubiri maswala ya Upendo, Amani katika familia zetu.

"Na ulinzi wa haki za binadamu unaanzia katika familia, Ulinzi wa haki za binadamu unaanzia kwa mtu mmoja mmoja, unakuja kwa familia, kaya, taifa na duniani kote, kwa hiyo viongozi wa dini wana nafasi kubwa na wanasikilizwa na watu wanawaelewa hivyo sisi tunawaona viognozi wa kidini kama watu wa muhimu sana katika ulinzi na utetezi wa haki za binadamu nchini na ni muhimu kushirikiana nao” amesema Olengurumwa

Aidha amesema hatua hiyo ni mwendelezo wa zile zinazochukuliwa na mtandao wa Watetezi wa haki za Binadamu, kushirikiana na taasisi mbalimbali nchini katika kuhakikisha ulinzi na utetezi wa haki za binadamu unazingatiwa na kusimamiwa katika kila Sekta ili kwa pamoja kujenga Tanzania iliyo bora inayozingatia ulinzi na utetezi wa haki za binadamu.

Mafunzo hayo yalifanyika katika Hotel ya Uhuru, iliyopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro, imekutanisha viongozi wa dini takribani Arobaini (40) kutoka katika Kamati za Dini Mbalimbali za mikoa ya Manyara, Dodoma pamoja na Kilimanjaro.

Katika Semina hii Viongozi wa dini wamejifunza namna mbali mbali za kufanya ufuatiliaji, ukusanyaji na utunzaji taarifa za masuala ya haki za binadamu, kutambua na kulinda haki za binadamu, kuwalinda wapigania haki hizo pamoja na kujifunza namna gani wanaweza kushiriki kutatua matatizo ya kijamii hasa katika maswala ya uvunjifu wa haki za binadamu.

Habari Kubwa