Watilii kutoka Asia na Ulaya wamiminika Tanzania

05Aug 2020
Allan lsack
HAI
Nipashe
Watilii kutoka Asia na Ulaya wamiminika Tanzania

Jumla ya watalii 177 kutoka mataifa mbalimbali ya Ulaya na Asia, wameendelea kuingia nchini Tanzania, kutembelea vivutio vya utalii, baada ya mashirika ya ndege kurudisha rasmi safari zake.

Watalii 177, kutoka mataifa ya Ulaya na Asia wakiwasili jana usiku majira ya saa 2:15, katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), na ndege ya shirika la Uholanzi "KLM" PH-BQB aina ya Boeing 777. PICHA : Allan lsack

Awali mashirika ya ndege ya kimataifa na yasiyo ya kimataifa yalisitisha safari zake kwenye nchi mbalimbali duniani kutokana na maambukizi ya ugonjwa wa covid-19.

Mashirika ya ndege ambayo hadi sasa yamesharudisha safari zake nchini Tanzania, ni pamoja na shirika la ndege la Rwanda Air,Ethiopia, Qatar, Emirates na shirika la ndege la nchini Uholazi la KLM.

Akizungumza wakati wa hafla fupi,ya kuwapokea watalii 177, iliyofanyika katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Anna Mghwira, alisema kuingia kwa watalii hao, hapa nchini kumeonyesha hali ya ushindi dhidi ya ugonjwa wa corona.

Alisema watalii hao,waliowasili uwanjani hapo kwa ndege ya Shirika  la Uholanzi “KLM”, PH-BQB aina ya Boeing 777.

Mgwira alisema, kurejea kwa safari za ndege hizo, kumeithibitishia dunia kwamba wananchi wa Tanzania wameishinda hofu ya ugonjwa wa covid-19.

Alisema kurejea kwa safari za ndege hapa nchini, kumeonyesha wazi kuwa maambukizi ya ugonjwa wa corona  yamekwisha, hivyo ni wakati wa wananchi kuendelea na shughuli za uzalishaji mali.

“Kuja kwa watalii hawa ni ishara ya ushindi mkubwa,ni ishara njema ya amani na upendo, hivyo nawaomba wananchi popote walipo watambue kuwa Tanzania ni sehemu salama ya utalii,”alisema Mgwira.

Naye Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Usimamizi na Uwendeshaji wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro(KADCO),Christine Mwakatobe, alisema Jana majira ya saa 2:15 usiku waliwapokea watalii 177, wakitokea kwenye mataifa ya  Ujerumani,Uingereza,Ufaransa na wengine  nchi za bara la Asia.

Hata hivyo, alisema kurejea kwa safari za ndege hiyo, kumetokana na serikali ya Uholanza na ufaransa, ambao ndio wamiliki wa ndege hiyo, kuridhika na jitihada za serikali ya Tanzania katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa corona.

“Kuja kwa ndege hii, kumetoa matumaini kwa watanzania na mataifa yote duniani kuwa Tanzania ipo salama ndio sababu wageni wengi wanaendelea kuja kwa wingi katika mbuga zetu za utalii,”alisema Mwakatobe.

Mwakatobe alisema, Agosti 2 mwaka huu, walipokea ndege ya shirika la RwandAir 9XR- WL, Juni 01 mwaka huu, walipokea ndege ya shirika la Ethiopia, Julai 30 walipokea  ndege ya shirika la Qatar, Agosti 01 walipokea ndege ya Crystal  P4_XTL.

Akizungumza kwa niaba ya watalii waliowasili uwanjani hapo, Getrude Boldemann, raia kutoka nchi ya Ujerumani, alisema wamefurahishwa sans na kauli ya Rais John Magufuli, kwamba Tanzani hakuna ugonjwa wa corona, ndio sababu wamekuja kutalii kwenye mbuga za wanyama.

Aidha alisema, nchi ya Tanzania ni sehemu nziri ya kuvutia na kila mtu anamatamanio ya kufika kutokana na kuwa na vivutio vingi vya utalii.

Habari Kubwa