Watiwa mbaroni tuhuma kwa mauaji mtendaji Dar

13Oct 2021
Maulid Mmbaga
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watiwa mbaroni tuhuma kwa mauaji mtendaji Dar

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linawashikilia watu watatu kwa tuhuma za kuhusika na mauaji ya kikatili dhidi ya Ofisa Mtendaji wa Mtaa wa Mbezi Msumi wilayani Ubungo, Kelvin Mowo.

Ofisa huyo anadaiwa kuuawa kwa kukatwa mapanga akiwa ofisini kwake juzi, chanzo kikidaiwa kuwa mgogoro wa ardhi.

Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo, Jummane Muliro alisema jana kuwa walikuwa wamekamata watu watatu kwa tuhuma za mauaji hayo, lakini hakuwa tayari kuweka bayana majina yao kwa sababu za kiupelelezi.

“Wakati mtendaji huyo akiwa anatimiza majukumu yake katika ofisi ya mtaa, waliingia watu wanne ambao ni sehemu ya mgogoro huo na mmoja wao alitoa panga na kumjeruhi mtendaji huyo ambaye baadaye alivuja damu na kukimbizwa hospitalini lakini alipoteza maisha.

"Watuhumiwa watatu wamekamatwa na wengine wote ambao ni sehemu ya tukio hili watakamatwa na watafikishwa mahakamani kama sehemu ya hatua muhimu za kisheria," alisema Muliro.

Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makala, jana alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha watuhumiwa wote waliohusika kutekeleza mauaji hayo wanakamatwa na kufikishwa katika vyombo vya sheria.

“Kuchukua sheria mkononi ukajipa haki hiyo wewe na kuondoa maisha ya mtu asiye na hatia, sio aliyeuza ardhi, bali yuko pale katika majukumu ya kutenda haki na wewe ukaiharakisha kuipata haki yako kwa kutoa uhai wa mtu mwingine, hilo ni jambo ambalo si sahihi na tukio hilo sio zuri hata kidogo.

“Nikiwa kama Mwenyekiti wa Ulinzi na Usalama, nimeelekeza Jeshi la Polisi kuwasaka wahalifu wote waliohusika na kufikishwa katika vyombo vya sheria, na wananchi kama mnajua kuna taarifa zozote zitakazosaidia watu hao kupatikana zitoeni na tutahakikisha wote waliohusika wanakamatwa," alisema.

Habari Kubwa