Watorosha makontena 11,000 Bandari kizimbani kesho

07Feb 2016
Christina Mwakangale
Nipashe Jumapili
Watorosha makontena 11,000 Bandari kizimbani kesho

WATUMISHI saba kati ya nane wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) ambao wanatuhumiwa kutorosha makontena 11,019 na magari 2,019 kutoka bandari kavu (ICD) bila kulipiwa ushuru, wanatarajiwa kufikishwa mahakamani kesho baada ya upelelezi wa kesi hiyo kukamilika.

Awali, watumishi 15 wa TPA wakiwamo waliokuwa wakishika nafasi mbalimbali za juu ndani ya mamlaka hiyo, walitajwa na Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kuwa wanatuhumiwa kushiriki katika utoroshaji wa makontena na magari hayo kutoka katika bandari kavu saba bila ya kulipa ushuru wa Bandari. Kamanda wa Kanda Maalum jijini Dar es Salaam, Simon Sirro aliiambia Nipashe juzi kuwa, wafanyakazi hao wanakabiliwa na tuhuma za kuipotezea serikali mapato ya Sh. bilioni 48.55. “Tunatarajia kuwafikisha mahakamani Jumatatu kwa sababu upepelezi tuliokuwa tukiufanya umeshakamilika,” alisema Kamanda Sirro. Januari 30, majira ya usiku, taarifa za kukamatwa kwa watumishi hao zilisambaa katika mitandao ya kijamii kuhusiana na suala hilo na alipiulizwa na Nipashe, Meneja Mawasiliano wa TPA, Janet Ruzangi, alikiri kuwa taarifa hiyo imetoka kwenye ofisi yake. Ruzangi alisema mfanyakazi mmoja hajapatikana na Jeshi la Polisi linaendelea kumsaka ili afikishwe katika vyombo vya sheria. Alidai mtuhumiwa huyo ni Happygod Naftali, ambaye alishaacha kazi TPA baada ya viongozi kuanza kufuatilia suala la makontena. Watumishi waliokamtwa na polisi, kwa mujibu wa Ruzangi, walikuwa ni Aron Lusingu, Amani Kazumari, John Mushi, Valentine Sangawe, Bonasweet Kimaina, Zainab Bwijo na Nathan Edward. Watumishi hao wanaungana na watumishi wengine saba, ambao ni John Elisante, Leticia Masaro, Christina Temu, Merina Chawala, Adnan Ally, Masoud Suleiman (Kova) na Benadeta Sangawe waliokamatwa mapema na kuhojiwa kuhusu sakata hilo. Kuhusu mawakala 280 waliopewa siku saba wawe wamewasilisha maelezo yao makao makuu ya TPA kuhusu namna walivyohusika kulipia makontena hayo, Ruzangi alisema mamlaka yake inajipanga kutoa taarifa kamili juu ya suala hilo. “Tunaendelea kuandaa taarifa ya kilichotokea na kilichobainika kuhusu mawakala hao… tutatoa taarifa hivi karibuni,” alisema Meneja Mawasiliano huyo. Baada ya Rais John Magufuli kuingia madarakani, uongozi wake ulianza kuibua matukio kadhaa ya ufisadi kupitia operesheni ameiita ‘kutumbua majipu’. Ufisadi huo ni pamoja na uliokuwa ukifanywa kwenye Bandari ya Dar es Salaama kwa kupitisha makontena bila kulipiwa kodi wala ushuru, huku washiriki wakiwa ni pamoja na wafanyakazi wa TPA, mawakala pamoja wa forodha na wafanyakazi wa Mamlaka ya Mapato (TRA). Kwa mara ya kwanza upotevu wa makontena 349 uligundulika baada ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kufanya ziara bandarini na kubaini makontena hayo kutolewa bandari kavu bila kulipiwa kodi. Upotevu huo uliwaponza vigogo wa TRA, akiwamo Kamishna Mkuu Rished Bade, na makamishna wengine kadhaa waliosimamishwa kazi na baadhi yao kufikishwa mahakamani, akiwemo aliyekuwa Kamishna wa Forodha, Tiagi Masamaki. Baadaye Majaliwa alibaini upotevu mwingine wa makontena 2,431 yaliyoondolewa bandari kavu bila kulipiwa ushuru wa Bandari. Katika sakata hilo, baadhi ya mawakala wa forodha walifungiwa kufanya biashara na TPA. Kashfa ya mwisho ni kupotea kwa makontena hayo 11,019 na magari 2,019.

Habari Kubwa