Watoto 200 jamii ya kimasai kuanza masomo ya sekondari

06Jan 2019
Na Mwandishi Wetu
SIMANJIRO
Nipashe Jumapili
Watoto 200 jamii ya kimasai kuanza masomo ya sekondari

WANAFUNZI 200 wa jamii ya wafugaji wa Kimasai waliochaguliwa kuingia kidato cha kwanza wanatarajia kuanza masomo kesho katika shule ya Sekondari ya Emboret, wilayani hapa.

WATOTO WA KIMASAI WALIOFAULU KWENDA KIDATO CHA KWANZA KUANZA MASOMO KESHO

Wanafunzi hao wanaanza masomo licha ya ujenzi wa vyumba vitatu vya madarasa katika shule hiyo kuendelea.

 

Akikagua maandalizi ya ujenzi huo, Mwenyekiti wa shirika lisilokuwa la kiserikali la ECLAT Development Foundation, Peter Toima, alisema shirika lake litatumia Sh.  milioni 91 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba hivyo.

 

Toima alisema shirika lake ambalo limekuwa likiboresha miundombinu ya shule hiyo tangu mwaka 2015, linatarajia kuchukuwa miezi miwili na nusu kukamilisha ujenzi wa vyumba hivyo vitatu.

 

“Kiasi hicho cha Sh. milioni 91 zitatumika kujenga vyumba hivyo pamoja na samani ambazo ni viti na meza. Ndani ya kipindi kisichozidi miezi mitatu ujenzi utakuwa umekamilika,” alisema.

 

Toima alisema wanafunzi wote wanaochaguliwa kuendelea na masomo, watatumia vyumba vya muda kama madarasa kutokana na shule hiyo kuwa na majengo ya kutosha ambayo yanatumika kwa shughuli zingine za kitaaluma.

 

Alitaja vyumba hivyo kuwa ni pamoja na maktaba, maabara ya kompyuta, maabara tatu za masomo ya sayansi na ofisi za walimu  ambazo alisema pia tayari kuna meza na viti zaidi ya 650 vya bwalo.

 

Mwenyekiti huyo alisema kuwa shirika lake hutenga Sh. milioni 500 kila mwaka kwa ajili ya kuimarisha miundombinu ya shule hiyo na kwamba kazi hiyo itaendelea mpaka mwaka 2020.

 

Alisema katika kipindi cha miaka mitatu, wamejenga  nyumba za walimu, vyumba vya maabara, kuweka umeme wa nishati ya jua, kuchimba kisima kirefu cha maji na kuweka mtambo wa gesi ya kinyesi.

 

Toima alisema uimarishaji wa miundombinu ya sekondari hiyo unakwenda sambamba na uboreshaji wa shule saba za msingi katika eneo la kata hiyo.

 

Alisema uboreshaji huo katika shule za msingi unahusisha ujenzi wa shule mpaka katika maeneo ambayo yana shule zenye idadi kubwa ya wanafunzi, ujenzi wa madarasa mapya na vyoo vipya na vya kisasa.

 

“Katika kufanyakazi hii tuna mkataba wa ushirikiano na serikali ya wilaya ya Simanjiro na mara tunapokamilisha ujenzi tukabidhi kwa serikali.

 

Mwalimu wa shule hiyo ya sekondari, Samwel Kaitua, alisema kuimarika kwa miundombinu kumewezesha shule hiyo kufanya vizuri na kushika nafasi ya kwanza katika wilaya na nane katika mkoa katika matokeo ya kidato cha nne kutoka nafasi ya mwisho mwaka 2015.

 

Katibu Tawala wa Mkoa wa Manyara, Missaile Mussa, amewaagiza wakurugenzi na watendaji wa halmashauri za wilaya katika mkoa huo kuhakikisha wanafunzi 5,000 waliokosa nafasi kati ya wanafunzi 21,453 walifaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2018 wanaendelea na kidato cha kwanza.

 

Shule ya sekondari ya Emboret licha ya kuwa ya kidato cha kwanza mpaka nne  ndiyo ya shule ya pekee ya serikali katika wilaya ya Simanjiro yenye kidato cha tano na cha sita.

 

 

Habari Kubwa