Watoto 2,600 washindwa kujiunga masomo sekondari

12Jan 2019
Paul Mabeja
Dodoma
Nipashe
Watoto 2,600 washindwa kujiunga masomo sekondari

WANAFUNZI 2,610 kati ya 8,038 waliochaguliwa kujiunga na masomo ya kidato cha kwanza kwa mwaka huu katika Halmashauri ya jiji la Dodoma, wameshindwa kujiunga kutokana na upungufu wa vyumba vya madarasa.

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, picha mtandao

Hayo yalibainishwa juzi kabla ya kuanza kwa ziara ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Binilith Mahenge, kutembelea shule zenye uhaba wa vyumba vya madarasa mkoani hapa.

Kutokana na taarifa hiyo, Dk. Mahenge alisema hatakubali kuona halmashauri yoyote ndani ya mkoa wake ikihangaika na ujenzi wa vyumba vya madarasa katika hatua za mwishoni baada ya matokeo kutoka.


“Yapo mambo ambayo tusikubali kuyafanya dakika za mwisho kwa mfano vyumba vya madarasa, matundu ya vyoo na madawati, sababu tunajua wale watoto wanaofanya mtihani mwezi wa tisa wapo watakaofaulu na watachaguliwa na watahitaji vyumba vya madarasa , vyoo nyumba za walimu na vitu vingine,” alisema.

“Sasa maelekezo yangu ni kuwa vyumba vyote vinatakiwa kukamilika na kuanzia sasa sitakubali katika mkoa wangu kuona halmashauri inahangaika dakika za mwisho,” aliongeza.

Alimuagiza Mkuu wa Wilaya ya Dodoma, Patrobas Katambi, kuhakikisha anakaa na viongozi wa serikali za mitaa ili wakawahamasishe wananchi kutambua umuhimu wa watoto wao kuripoti katika shule walizochaguliwa.

“Kila kata kuna shule hivyo mtakuwa mmepata orodha ya wanafunzi waliochaguliwa na hawajaripoti hivyo muwaelekeze wenyeviti wa serikali za mitaa kwamba watoto hao waripoti shuleni na wasiporipoti nafasi zao zitachukuliwa na wanafunzi wengine ambao walifaulu lakini wamekosa nafasi ya kuchaguliwa kutokana na upungufu wa madarasa,” alisema.

Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dodoma, Hidaya Maeda, alisema wameamua kujenga madarasa 40 badala ya 52 yanayohitajika kulingana na fedha zilizotolewa.

“Ni kweli mahitaji yetu ni madarasa 52 lakini kwa mpango wa haraka wa sasa ni kwamba tumejipangia kukamilisha madarasa 40, kwa maana tunapewa mgawo kila kota kwa hiyo kota hii ya Januari kuna hela nyingine tutapewa, hivyo tutakamilisha hayo madarasa mengine, kufikia Februari 9, 2019 yawe yamekamilika,” alisema.

Habari Kubwa