Watoto 450,000 kupatiwa chanjo ya polio Shinyanga

18May 2022
Marco Maduhu
SHINYANGA
Nipashe
Watoto 450,000 kupatiwa chanjo ya polio Shinyanga

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga, Sophia Mjema, amezindua zoezi la utoaji chanjo ya matone ya polio kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano, ili kuwakinga na ugonjwa wa kupooza utokanao na virusi vya polio.

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema akimpatia mtoto Chanjo ya Polio wakati akizundua zoezi hilo mkoani Shinyanga la utoaji wa Chanjo kwa watoto waliochini ya umri wa miaka mitano.

Zoezi hilo la utoaji chanjo ya polio mkoani Shinyanga, limezinduliwa leo na litahimishwa Mei 21, 2022.

Mjema akizungumza wakati wa uzinduzi huo amewasihi wazazi mkoani humo, kuwapeleka watoto wao kwa wingi kupata matone ya chanjo hiyo ambayo itawakinga dhidi ya ugonjwa wa kupooza.

“Niwatoe hofu wazazi wa mkoa huu wa Shinyanga, chanjo hii ya polio ni salama kabisa na haina madhara yoyote, hivyo wapelekeni watoto wenu wakapate chanjo na kubaki kuwa salama, sababu ugonjwa huu upo tu hapa nchi ya jirani Malawi,”amesema Mjema na kuongeza kuwa;

“Ugonjwa huu wa kupooza una ambukizwa kwa kirusi cha polio kwa kula chakula, kunywa maji machafu au kinyesi, na watoto ndiyo wapo katika hatari kubwa kutokana na kula hovyo hasa wanapokuwa wakicheza, na ndiyo maana wanapatiwa chanjo,”ameongeza 

Kwa upande wake Carle Lyimo kutoka Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), amesisitiza kuwa chanjo hiyo ni salama, na kuelezea kuwa imekuja kwa ajili ya kumkomboa mtoto wa Mtanzania kutokana na ugonjwa huo kuathiri watoto wa nchi jirani ya Malawi.

“Ugonjwa huu upo nchi jirani ya Malawi, na kuna muingiliano mkubwa wa kibiashara, na ndiyo maana tunasisitiza sana watoto wetu wapatiwe Chanjo ya Polio,”amesema Lyimo.

Mganga Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Dk. Yudas Ndugile amesema chanjo hiyo inatarajia kufikia watoto 450,000 walio na umri chini ya miaka mitano, na itatolewa kwenye vituo vya afya, maeneo yenye mikusanyiko ya watu, pamoja na nyumba kwa nyumba ili kufikia malengo kusudiwa.

Habari Kubwa