Watoto kortini tuhuma kughushi saini ya baba

29Jul 2021
Kulwa Mzee
Dar es Salaam
Nipashe
Watoto kortini tuhuma kughushi saini ya baba

WATOTO watano wa familia moja, wamefikishwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu kwa tuhuma za kughushi saini ya baba yao katika kuhamisha umiliki wa ardhi.

Washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi, Joseph Lwambano, na kusomewa mashtaka na Wakili Neema Mushi.

Akisoma mashtaka hayo, Wakili Mushi aliwataja washtakiwa kuwa ni Saidi Athumani, Tufaa Athumani, Fatuma Athumani, Amal Athumani na Nimiit Athumani.

Washtakiwa wanadaiwa kula njama kutenda kosa Agosti mwaka 2016, Mtaa wa Lumumba wilayani Ilala.

Inadaiwa katika kipindi hicho, kwa nia ya kudanganya, walighushi saini ya Ally Athumani wakionyesha ilikuwa halali na ilitolewa na Ally Athumani wakati siyo kweli.

Wakili Mushi alidai katika kipindi hicho washtakiwa walighushi saini ya baba yao katika uhamisho wa umiliki wa ardhi wakionyesha hayo yalifanywa na Ally Athumani wakati siyo kweli.

Upande wa Jamhuri ulidai upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, hivyo kesi kuahirishwa hadi Agosti 11, mwaka huu kwa kutajwa.

Mahakama ilitoa masharti ya dhamana ambapo kila mshtakiwa alitakiwa kuwa na wadhamini wawili wa kuaminika, wanne wakifanikiwa kupata dhamana huku mshtakiwa wa kwanza aliyeshindwa kutimiza masharti ya kuwa na wadhamini wawili.

Katika hatua nyingine, mbele ya Hakimu Ritha Tarimo, mshtakiwa Frank Mahelela alisomewa mashtaka ya wizi akiwa mtumishi.

Inadaiwa kati ya Mei 28, mwaka 2019 na Septemba 30, 2019, maeneo ya Ofisi ya Kimataifa ya Wahamiaji iliyoko Masaki, akiwa mhasibu, aliiba Dola za Marekani 156,000 sawa na Sh. milioni 358.8, mali ya mwajiri wake, fedha zilizokuja kwenye umiliki wake kupitia ajira yake.

Mshtakiwa anadaiwa kughushi kadi ya mpigakura yenye jina la Airi Asa Salaam kwa kujifanya ilikuwa halali na ilitolewa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC).

Inadaiwa kuwa Mei 28, 2019, katika Benki ya Azania, Tawi la Masdo, kwa nia ya kudanganya, aliwasilisha kitambulisho hicho kwa Waida Abubakar ambaye ni mtoa huduma wa benki hiyo kwa kudai ni nyaraka halali wakati siyo kweli.

Inadaiwa katika Benki ya Azania, kwa nia ya kudanganya, alijitambulisha kama Airi Asa Salaam kwa Wahida ambaye ni ofisa huduma wa wateja, kitu ambacho siyo kweli.

Upelelezi wa kesi hiyo haujakamilika, washtakiwa wanatarajia kuletwa leo kwa ajili ya masuala ya dhamana, Wakili aliyewakilisha Upande wa Jamhuri ni Esther Martin.

Habari Kubwa