Watoto milioni 3.5 wako nje ya shule - Ripoti

06Mar 2017
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Watoto milioni 3.5 wako nje ya shule - Ripoti

TANZANIA ina jumla ya vijana wenye umri wa miaka kati ya saba na 17 milioni 3.5 waliopo nje ya shule, Ripoti ya Taasisi ya Watu Wazima (TEWW) inaonyesha.

Kati ya vijana hao, milioni 2.5 wanahitaji elimu ya sekondari na milioni moja, wanahitaji elimu ya msingi.

Naibu Mkurugenzi wa TEWW, Dk. Kassim Nihuka, takwimu za taasisi hiyo ni za mwaka 2012.

Dk. Nihuka alisema tatizo la vijana na watu wazima waliokosa elimu ya sekondari, ni kubwa lakini si kwa Tanzania tu, bali kwa nchi zote zilizopo katika ukanda wa Kusini mwa Jangwa la Sahara.

“Vijana wanaomaliza elimu ya msingi na kupata alama ufaulu chini ya 100 (kati ya 250), wamekuwa wakiachwa kwenda sekondari katika mikoa mbalimbali isipokuwa wale ambao wazazi wao wana uwezo wa kuwapeleka shule za sekondari za binafsi ambazo gharama zake ni za juu,” alisema Dk. Nihuka.

Alisema programu iliyoanzishwa na TEWW imekusudia kuwawezesha wanafunzi waliomaliza darasa la saba ambao hawakupata nafasi ya kuendelea na masomo ya sekondari na wanahitaji kumaliza elimu hiyo.

Dk. Nihuka alisema programu hiyo inaendeshwa katika majengo ya shule za msingi na sekondari za serikali 83 na wadau 337 nchini.

Alisema hadi kufikia sasa, vijana na watu wazima 95,140 wamenufaika na masomo hayo kuanzia mwaka 2010 hadi 2016.

Aidha, Dk. Nihuka aliongeza kuwa programu hiyo pia imewalenga wanafunzi waliomaliza masomo ya Mpango wa Elimu ya Msingi kwa Walioikosa (Memkwa) na waliomaliza masomo ya sekondari, lakini hawakufanya vizuri na wangependa kurudia mtihani wa taifa wa kidato cha nne.

Kwa mujibu wa Dk. Nihuka, kupitia programu hiyo, masomo hutolewa katika hatua kuu tatu.

Alizitaja hatua hizo kuwa ni masomo ya kidato cha kwanza na pili, masomo ya kidato cha tatu na nne na hatua ya mwisho inabeba masomo ya kidato cha tano na sita.

“Katika hatua ya kwanza, mlengwa anasoma kwa kipindi cha mwaka mmoja na hivyo kuwa na sifa ya kufanya mtihani wa maarifa. Masomo yanayotolewa katika hatua hii ni Historia, Jiografia, Kiingereza, Kiswahili, Hisabati, Biolojia na Uraia,” alisema Dk. Nihuka.

Alifafanua kuwa mlengwa wa hatua ya pili anatakiwa kusoma kwa kipindi cha mwaka mmoja na ndipo atakuwa na sifa ya kufanya mtihani wa kidato cha nne uliondaliwa na Baraza la Mitihani la Taifa (Necta).

Kuhusu hatua ya mwisho ya programu hiyo, Dk. Nihuka alisema masomo mahsusi yanayotolewa katika tahasusi za HGL (Historia, Jiografia na Lugha), HKL (Historia, Kiswahili na Lugha), HGK (Historia, Jiografia na Kiswahili) pamoja na HGE (Historia, Jiografia na Uchumi), na mlengwa katika hatua hiyo anaweza kusoma kwa zaidi ya mwaka mmoja hadi pale atakapokuwa amejiandaa vya kutosha kufanya mtihani wa maarifa au ule wa Necta.

Alifafanua kuwa masomo hayo yanatolewa kupitia mafunzo ya ana kwa wakati wa jioni na mlengwa atajisomea moduli na vitabu na matumizi ya teknolojia za kujifunzia kama vile elimu mtandao kupitia machapisho huria ya kielimu.

Kuhusu gharama za masomo hayo, Dk. Nihuka alisema viwango vya ada vinavyotozwa na TEWW katika elimu ya sekondari hutofautiana na vituo vinavyoendeshwa na wadau.

Habari Kubwa