Watoto njiti wasababisha msongamano Muhimbili

14Feb 2016
Romana Mallya
Nipashe Jumapili
Watoto njiti wasababisha msongamano Muhimbili

UKOSEFU wa huduma ya kuwahudumia watoto njiti katika hospitali mbalimbali nchini, umesababisha msongamano wa wanawake wanaolala chini Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, jijini Dar es Salaam.

Mkurugenzi wa Wauguzi na Ubora hospitali hapo, Agness Mtawa, akizungumza na Nipashe kuhusu changamoto ya wanawake kulala chini, alisema miongoni mwa matatizo wanayosababisha ni ongezeko la watoto njiti wanaopokelewa hospitalini hapo kutoka hospitali nyingine nchini.

Mtawa alisema hadi juzi mchana jumla ya watoto 114 kutoka mikoa tofauti walikuwa kwenye chumba maalum kwa ajili ya kupatiwa huduma ili waweze kukuwa.

“Tunaposema tunawatoto 114 maana yake wapo na mama zao 114 hawa ni wale wanaopokelewa kutoka hospitali mbalimbali nchini kutokana na huko kukosekana huduma hii ya watoto hawa, lakini hapo kumbuka tunawagonjwa wengine wodini ambao wameletwa kujifungua na wengine wamehamishiwa hapa kutokana na matatizo, sasa kwa nini watu wasilale chini,” alisema na kuongeza:

“Tunachokifanya wanawake waliowaleta watoto njiti kwa sababu wao hawana matatizo huwa wanalala kwenye magodoro. Huwezi kumlaza chini mtu aliyetoka kwenye upasuaji au mwenye tatizo, huwa tunaangalia na tatizo la mtu, hatupendi walale chini lakini kwa sababu wanakuja kutokana na matatizo hawana jinsi,”alisema.

Aliongeza kuwa, hata wao kitaaluma inawakwaza kuwahudumia wagonjwa wanaolala chini lakini kwa sababu ya changamoto ya eneo la kuweka vitanda hospitalini hapo hawana jinsi.

“Tunapenda kila tunayemhudumia awe kitandani na inakuwa rahisi kumpa huduma kuliko yule aliyelala chini lakini hatumaanishi aliyelala chini anapata huduma tofauti na yule wa kitandani,”alisisitiza.

Aidha, alisema kutokana na wingi wa watoto hao, wameanzisha huduma ya ‘kangaroo’ ambapo mama analala na mtoto wake kifuani.

“ Hadi sasa jumla ya kina mama 17 wanalala na watoto wao kifuani, kule kwenye chumba maalum cha watoto njiti kutokana na kuwa wengi, wanalala wawili wawili kwa kuwatenganisha na nguo, nataka uone jinsi tatizo lilivyo kubwa la ufinyu wa rasilimali nafasi,” alisema.

Mbali ya changamoto hiyo ya rasilimali nafasi, Mtawa alitaja nyingine kuwa ni mashine za kupimia BP ambazo sasa hazina ubora na kwamba zinakufa haraka.

“Hatuna mashine za kupimia presha ( BP) za kutosha na hii inatokana na wingi wa wagonjwa , lakini hata zilizopo hazina kiwango unatumia kwa wagonjwa 250 na kwa muda wa wiki mbili unatupa wakati za awali zilikuwa zikihudumia wagonjwa wengi na zilikuwa zinakaa kwa miaka mitano,” alisema.

Alitaja vifaa vingine kuwa ni monitor mashine ambazo kwa sasa zipo chumba cha wagonjwa mahututi tu.

“Mashine ya Infusio Pump ambazo hutumika kupeleka dawa katika mshipa wa damu, mashine ya pulse Oxymeter inayotumika kupima kiasi cha hewa inayotumika kwa mgonjwa na mapigo ya moyo nazo ni chache,” alisema.

Habari Kubwa