`Watoto wanaoishi mazingira magumu wasinyanyaswe shuleni’

14May 2017
Robert Temaliwa
Nipashe Jumapili
`Watoto wanaoishi mazingira magumu wasinyanyaswe shuleni’

WALIMU na wanafunzi wameshauriwa kutowanyanyapaa watoto waliopoteza wazazi na kuishi katika mazingira magumu ili waweze kufanya vizuri shuleni katika masomo yao.

Wito huo ulitolewa juzi wilayani hapo na Mkurugenzi wa kituo cha kulelea watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu cha Amani Orphance kilichopo chini ya Shirika la Empowering Children and Organization (ECCO), Margareth Mwegalawa, wakati akizungumza na Nipashe kuhusu adha wanayoipata watoto shuleni.

Mwegalawa alisema watoto wao wanaowalelea katika kituo hicho wanapata wakati mgumu wanapokuwa shuleni kutokana na kubaguliwa kwa kutopewa ushirikiano mzuri na baadhi ya wanafunzi wenzao na hata baadhi ya walimu.

Alisema kuwanyanyapaa watoto yatima na wanaoishi katika mazingira magumu kunawapa unyonge kwa kuwa hawakupenda kuwa katika hali hiyo bali ni kwa mapenzi ya Mwenyezi Mungu.

"Watoto yatima na ambao si yatima wote ni watoto, hivyo wanatakiwa kupendwa kwa kiwango kinacholingana ili kutowafanya watoto ambao ni yatima kujisikia vibaya, hali ambayo inaweza kusababisha wasifanye vizuri katika masomo yao, licha ya kuwa na bidii ya kusoma," alisema.

Aliongeza kuwa walimu wanaoonyesha ubaguzi kwa kutotoa ushirikiano kwa wanafunzi ambao ni yatima, ndiyo chanzo kikubwa cha wanafunzi wengine kuwanyanyapaa.

Mwegalawa alisema kutokana na adha kubwa ya watoto wao kunyanyapaliwa na wenzao shuleni wakiwamo baadhi ya walimu, wameanza mikakati ya ujenzi wa shule ya kuanzia chekechea hadi sekondari huku wakitegemea msaada wa wadau wengine wa elimu.

"Tutaomba serikali kuu na wadau wengine wa elimu watusaidie kutimiza mipango yetu ya ujenzi wa shule kwa ajili ya watoto wetu ambao wanapata elimu katika mazingira magumu kutokana na  kunyanyapaliwa na wenzao, " alisema.