Watu saba wauawa na Tembo Longido

04Dec 2019
Daniel Sabuni
Arusha
Nipashe
Watu saba wauawa na Tembo Longido

Inaelezwa kuwa watu saba wameuawa na Tembo kwa nyakati tofauti tangu januari mwaka huu katika vijiji vya Kimokoa, Sinya na Ngalehani wilayani Longido.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Frank Mwaisumbe aliyasema hayo wakati akizungumza na Nipashe kwa simu, na kusema vifo hivyo  vimesababishwa na muingiliano wa shughuli za kibinadamu na wanyama katika vijiji hivyo.

Amesema kuwa matukio mengi ya vifo vya wanakijiji wa maeneo hayo yametokea ambapo wakazi hao walipokuwa wakienda kuchota maji, kutafuta kuni na kuchunga mifuko na kupelekea kushambuliwa na Tembo.

“Utakuta binadamu wanatafuta mahitaji na Tembo nao wanafika katika kijiji kutafuta maji na hata kutembelea maeneo ya kihistoria sasa wanapokutana na wanyama hao huanza kuwakimbiza na kuwashambulia na ndivyo ilivyotokea kwa wenzetu waliuoawa” amesema 

Amesema kuwa Tembo ana historia ya ajabu, kama wazazi wake walishapita au kupata huduma  sehemu fulani, hurithishana hivyo hata kama ni miaka 200 iliyopita watapita maeneo jayo hata kama ni mjini.

“Tumesikia hivi karibuni tembo walifika jijini Tanga na kuzuha tafrani, hali kama hiyo ndio ninayoizungumzia, hata kama kuna ukoo fulani au kabila fulani walihusika kwenye mauaji ya Tembo wanapopita wakanusa sauti au kukumbuka lugha ya kabila fulani waliohusika lazima walipizwe kisasi,…Tembo wanauwezo mkubwa wa kunusa na kukumbuka sautikwa kufuata kabila au harufu ya binadamu" amesema 

Hata hivyo Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na usalama wa Wilaya ya Longido amesema serikali kwa ujumla imechukua hatua kwanza kwa kutoa elimu kwa wanavijiji wanaoishi sehemu ya ushoroba wa wanyama kwa kushirikiana na TANAPA na kwamba watembee kwenye makundi ya watu wengi wakiambatana na mbwa ili kuwajulisha juu ya hatari ya tembo.

Amesema pia serikali inaepuka kujenga majengo ya huduma za  jamii kwenye eneo la ushoroba ili kuepuka mgongano zaidi kwa kuwa wanyama jamii ya tembo hawapendi sauti na makelele ya binadamu.

“Huduma hizi tunaziweka pembeni mwa eneo eneo ambalo halitaweza kuongeza kasi ya kugongana, mfano shule na hospitali tunaepuka kungena ndani ya eneo la vijiji ambavyo viko kwenye mapito ya wanayama” amesemaMwaisumbe.

Amesema kuepusha madhira hayo serikali kupitia miradi mipya ya maji iliotengewa milioni 107 imeanza kazi ya uchimbaji wa Marambo katika vijiji wilayani humo na manne kati ya sita tayari yamekamilika na mradi wa kupeleka maji katika mji wa Namanga uliotengewa Bilioni 3 toka serikali kuu utajenga Marambo mengi ili kupunguza mgongano.

Habari Kubwa