Watu 168 wawekwa karantini

03Apr 2020
Na Mwandishi Wetu
Songwe
Nipashe
Watu 168 wawekwa karantini

KATIKA kutekeleza maagizo ya serikali ya kuhakikisha wasafiri wote nje ya nchi zikiwamo zenye maambukizi zaidi ya virusi vya corona wanatengwa, wasafiri 84 kutoka Afrika Kusini wamewekwa karantini kwa muda wa siku 14 mjini Tunduma.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, picha mtandao

Wakati wasafiri hao wakizuiwa, habari kutoka Zanzibar zinasema watu 84 wakiwamo madaktari 27 waliokuwa wakiwahudumia wagonjwa wa corona, nao wamewekwa karantini, hivyo kufanya idadi ya waliofanyiwa hivyo kuwa 168.

Mkuu wa Mkoa wa Songwe, Brigedia Jenerali Nicodemus Mwangela, alisema hayo jana alipofanya ukaguzi wa maandalizi ya utayari wa kupambana na Corona kwa Mkoa wa Songwe hususani maeneo ya mipakani, kwenye halmashauri za Wilaya ya Ileje na Mji wa tunduma.

Alisema wasafiri hao ambao ni Watanzania 55 na raia wengine kutoka Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC), Afrika Kusini, Kenya na Uganda, walipoingia nchini kupitia mpaka wa Tunduma, walipimwa na kukutwa hawana dalili za corona.

Licha ya kuwa hawakuwa na dalili, lakini alisema kwa kuwa wametoka katika nchi yenye maambukizi zaidi wamewekwa katika karantini.

Alisema utaratibu huo ni kwa ajili ya kuwaaangalia ndani ya siku 14 na kama watakuwa hawana dalili za virusi vya Corona, wataruhusiwa kuendelea na safari zao.

Jenerali Mwangela aliwaagiza viongozi katika sekta mbalimbali kuendelea kutoa elimu ya namna ya kujikinga na corona na pia katika ofisi na taasisi zote usafi uzingatiwe likiwamo suala la kunawa mikono kwa maji na sabuni.

Pia aliagiza Jeshi la Polisi Mkoa wa Songwe kufanya msako katika maeneo ya stendi za mabasi endapo kutakuwa na raia kutoka katika nchi zenye maambukizi zaidi ya corona na wamepitia njia zisizo rasmi ili wawekwe karantini.

"Mpaka sasa tumewaweka karantini wasafiri 84 katika mpaka wa Tanzania na Zambia ambao wengi ni raia wa Afrika Kusini na Congo na kazi hii inaendelea kusimamiwa vilivyo," alisema.

Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, George Kyando, alisema jeshi hilo limepiga marufuku kwa mabasi kujaza abiria kuliko uwezo wa gari, kutokuwa na vitakasa mikono kwenye mabasi au maji na sabuni kwa ajili ya kunawa na marufuku ya mabasi kuanza safari bila kupuliziwa dawa.

Alisema yeyote atakayepuuzia marufuku hizo ambazo zimelenga kuweka tahadhari ya kutosambaza ugonjwa wa corona atakuwa anataka kusambaza ugonjwa kwa makusudi jambo ambalo ni kosa kisheria hivyo hatua kali zitachukuliwa dhidi yake.

"Nimewaagiza askali wangu wa usalama barabarani wasiruhusu basi kujaza abilia, bora izuiliwe kufanya hizo biashara na si kujaza abiria," alisema.

Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mji wa Tunduma, Dk. Enock Mwambalaswa, alisema wasafiri wote waliowekwa karantini wanapimwa mara mbili kwa siku ili kufuatilia maendeleo ya afya zao.

Alisema endapo atatokea mwenye dalili za virusi vya corona, hatua za haraka zitachukuliwa lakini hadi sasa wote wanaendelea vizuri na hakuna aliyebainika kuwa na viashiria vya ugonjwa huo.

Habari Kubwa