Watu 20 wakamatwa wakifanya biashara haramu ya fedha

24Oct 2019
Nebart Msokwa
KYELA
Nipashe
Watu 20 wakamatwa wakifanya biashara haramu ya fedha

JESHI la Polisi mkoani Mbeya limewakamata zaidi ya watu 20 wilayani Kasumulu mpakani mwa Tanzania na Malawi kwa tuhuma za kufanya biashara haramu ya kubadilisha fedha.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei.

Watu hao walikamatwa wakati wa Oparesheni ya kushtukiza iliyofanywa na Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na maofisa wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) na maofisa wengine wa vyombo vya usalama ambao walikuwa wamezingira maeneo mbalimbali ya mji huo.

Katika Oparesheni hiyo wafanyabiashara hao walikamatwa na zaidi ya Shilingi milioni 100 ambazo zilikuwa za mataifa mbalimbali zikiwemo fedha za Tanzania, Kwacha za Malawi na Dola za Marekani ambazo walikuwa wakizibadilisha kienyeji.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi, Ulrich Matei ambaye aliongoza oparesheni hiyo amesema biashara hiyo ni haramu kwa mujibu wa sheria zinazosimamia fedha hapa nchini.

Amewataka wafanyabiashara hao waliokuwa wanatumia mbinu mbalimbali kuwazuga maofisa hao ikiwemo kuandika maandishi yanayoonyesha kuwa kwenye maduka yao hayo wanafanya biashara ya fedha kwa njia za simu lakini kumbe humo ndani ndio wanafanya shughuli hizo.

“Nawashauri wafanyabiashara wote kuendelea kufuata taratibu, mtu yeyote anayetaka kubadilisha fedha za mataifa mbalimbali anatakiwa kwenda kwenye benki zetu au kwa watu wenye vibali maalumu na sio humu wanaofanya kienyeji,” amesema Kamanda Matei.

Aidha Kamanda Matei amesema biashara hiyo inafanyika kwenye mazingira ambayo sio salama kwa maisha yao hivyo wanazipiga marufuku kwa ajili ya maisha yao wenyewe.

Diwani wa Kata ya Njisi, Omary Mwinjuma amesema wananchi wa Kata yake ambao walikuwa wanafanya biashara hiyo hawana elimu ya kutosha kuhusu sheria ya fedha hivyo akaiomba serikali kuendelea kutoa elimu.

Amesema kitendo cha kuwakamata kwa kushtukiza kitawaathiri wao pamoja na familia zao, hivyo akaomba elimu iendelee kutolewa ili kuepuka kuwakamata wengine.

“Hii biashara imekuwa ikifanyika kwa kipindi kirefu na hatukuwa na uelewa wa kutosha kuhusu taratibu mpya za ubadilishaji wa fedha, hivyo kwa sasa pamoja na kuwakamata lakini nashauri pia elimu itolewe ili hata wananchi wa kawaida wajuwe maeneo sahihi ya kubadili fedha zao,” amesema Mwinjuma.

Amewataka Watanzania wanaofanya biashara kati ya Tanzania na Malawi kuendelea kufuata taratibu za nchi hizo mbili ili kuepuka kukumbana na mkono wa sheria.

Habari Kubwa