Watu wanne wa familia moja wafariki dunia kwa radi

24Sep 2021
Lilian Lugakingira
Muleba
Nipashe
Watu wanne wa familia moja wafariki dunia kwa radi

​​​​​​​WATU wanne wa familia moja ambao ni mume, mke na watoto wao wawili wamepoteza maisha kwa kupigwa na radi kutokana na  mvua iliyonyesha usiku wa kuamkia juzi katika kisiwa cha Bumbile kilichopo katika ziwa Victoria, upande wa Wilaya ya Muleba mkoani Kagera.

Mkuu wa wilaya ya Muleba Thoba Nguvilla, amesema kuwa mvua hiyo ilinyesha wakati watu hao wakiwa bado wamelala.

DC Nguvuli ametaja majina ya marehemu hao kuwa ni Slyvester Richard, mke wake Veronica Richard na watoto wao wawili wa kike ambao majina yao hayakupatikana haraka.

"Watu hawa ni wenyeji wa kisiwa cha Ukerewe Mkoa wa Mwanza, walikuja huku kutafuta maisha ambapo walikuwa wakilima na kuvua samaki, miili yao tayari imesafirishwa kwenda Ukerewe kwa shughuli za mazishi" amesema Nguvilla.

Akizungumza kwa njia ya simu mwenyekiti wa kitongoji cha Bulyo ambako tukio hilo limetokea Robert Musiibha amesema kuwa nyumba walimokuwa wamelala watu hao iliyokuwa imejengwa kwa mabanzi na kuezekwa kwa mabati, pia iliteketea kwa moto wa radi hiyo, na kuiomba serikali kuwapelekea mitego ya radi katika kisiwa hicho, ili kunusuru maisha yao.