Watu watano wafariki ajali ya basi na Lori Morogoro

16Aug 2019
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Watu watano wafariki ajali ya basi na Lori Morogoro

WATU watano wamefariki dunia na wengine 26 wamejeruhiwa usiku wa kuamkia leo baada ya basi la abiria la Safari Njema kugongana uso kwa uso na lori aina ya Tata mali ya kiwanda cha Tumbaku cha Alliance One katika eneo la Nanenane Manispaa ya Morogoro.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mtafungwa.

Akithibitisha kutokea ajali hiyo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Wilbroad Mtafungwa, amesema kuwa usiku wa kuamkia leo majira ya saa 7: 30 usiku Agosti 16,2019 imetokea ajali katika eneo la Nanenane barabara ya kutoka Dar es Salaam kuingia Morogoro ambapo basi la abiria la Safari Njema kugongana uso kwa uso na lori aina ya Tata mali ya kiwanda cha Tumbaku cha Alliance One.

"Usiku wa kuamkia leo Agosti 16, 2019,  ilikuwa ni saa 7:30 usiku katika eneo la Nanenane kwenye barabara ya kutoka Dar es salaam kuingia Morogoro gari lenye namba ya usajili T212 BMU ambalo ni basi la abiria aina ya Yutong mali ya kampuni ya Safari Njema lilikuwa likitokea Dar es salaam kwenda Dodoma usiku huo, lilivyofika kwenye eneo ilo dereva ali 'overtake' bila kuchukua tahadhari yoyote na kusababisha kugongana kwa ubavu na Gari lililokuwa na usajili T802 BUW ambalo ni Lori mali ya Kampuni ya Tumbaku ya Alliance, bahati mbaya watu wanne wamepoteza maisha akiwemo dereva wa lori," amesema Mtafungwa.

Kamanda Mtafungwa ameongeza kuwa dereva wa basi hilo la abiria baada ya ajali kutokea ametokomea kusikojulikana na juhudi za kumtafuta zinaendelea.

"Dereva wa ilo gari la abiria baada ya ajali ametoweka, hivyo basi jitihada za kumtafuta zinaendelea lakini sambamba na ilo kama atakuwa hajapatikana basi tutamtafuta mmiliki wake ili aonyeshe dereva alipo na hatua kali zitachukuliwa dhidi ya usalama barabarani,’’-amesema Mtafungwa.

Msimamizi wa zamu katika hospitali ya rufaa ya mkoa wa Morogoro, Nelly Nswila amezungumza na The Guardian Digital na kueleza kuwa amepokea miili ya watu watano na majeruhi 26 wa ajali ya basi na lori ilioyotkea usiku wa kuamkia leo.

Imeandikwa na Rahma Kisilwa, TUDARCO