Watu zaidi ya 800,000 wamepata chanjo ya Uviko-19

10Oct 2021
Na Mwandishi Wetu
Dodoma
Nipashe Jumapili
Watu zaidi ya 800,000 wamepata chanjo ya Uviko-19

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi, amesema hadi kufikia Jana Oktoba 9, 2021 watu zaidi ya 850,000 tayari wameshapata chanjo ya Uviko 19.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Afya Profesa Abel Makubi.

Profesa Makubi ametoa takwimu hiyo leo Oktoba 10, 2021 wakati akihamasisha waumini wa Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Katoliki jijini Dodoma ikiwa ni mwendelezo wa utekelezaji wa kampeni ya jamii harakishi na shirikishi inayoratibiwa na Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi).

Amesema kupitia kampeni hiyo watu wengi wameelimishwa na kupata uelewa wa chanjo na kuondoa zile sintofahamu ambazo zilikuwa zinaleta hofu katika jamii.

Akihutubia waumini kanisani, Profesa Makubi amesema chanjo za Uviko-19 zilizoletwa nchini ni salama kwa kuwa zimethibitishwa na wataalamu na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Profesa Makubi amesema mwitikio wa wananchi kujitokeza kupata chanjo baada ya kuanzishwa kampeni ni mkubwa na baada ya kuzinduliwa na Rais Samia Suluhu Hassan idadi ya waliochanjwa ilikuwa 28,000 nchi nzima lakini baada ya kampeni mpya ya jamii shirikishi, watu zaidi ya 850,000 wamechanjwa mpaka jana.

Profesa Makubi amesema kampeni ya jamii harakishi na shirikishi ilizinduliwa kwa lengo la kuhamasisha jamii kuchanja katika maeneo mbalimbali ikiwamo makanisa, misikiti, makundi mengine kama wanamichezo, makazini, masokoni, kwenye kaya na sehemu zote zenye mikusanyiko kuanzia mijini mpaka vijijini.

Habari Kubwa