Watuhumiwa kumuua mdogo wao wakigombania nyumba

03Jul 2020
Romana Mallya
Dar es Salaam
Nipashe
Watuhumiwa kumuua mdogo wao wakigombania nyumba

NDUGU wawili wa familia moja wanadaiwa kumuua mdogo wao, Mandela Malisa, kwa madai ya kumkuta amelala chumba cha baba yao mzazi ambaye kwa sasa ni marehemu, chanzo kikidaiwa kugombania nyumba ya urithi.

Tukio hilo lilitokea juzi Kata ya Sinoni, mkoani Arusha baada ya ndugu hao ambao ni dada wa marehemu kumshambulia ndugu yao na kitu cha ncha kali na kufariki dunia alipofikishwa hospitali.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa huo, Salum Hamduni, alipoulizwa kuhusu tukio hilo, alisema bado halijamfikia ofisini kwake.

Baba mkubwa wa marehemu, Emrod Malisa, alidai kabla ya tukio hilo, kijana aliyeuawa alimweleza kuwa amekosana na dada zake.

“Nilimwambia (marehemu) apumzike ili jioni (siku moja kabla ya mauaji hayo) niwaite dada zake, saa nane dada zake wakaja wenyewe kabla ya kuwaita, walikuja kushtaki kuwa wamekosana na ndugu yao.”

“Niliwaambia siwezi kusikiliza mashtaka ya upande mmoja nitawakutanisha siku ya Jumapili asubuhi (kesho kutwa) ili tuongelee hayo mambo tukaagana wakaondoka.”

Malisa alisema jana asubuhi alijulishwa kuhusu msiba huo na alipouliza chanzo akaambiwa kulitokea ugomvi baada ya Mandela kuhama kutoka chumba alichokuwa anakaa na kuhamia cha baba yake mzazi.

“Hawa dada zake wanasema hicho chumba kisiingiliwe na mtu, hii ni nyumba ya familia, hapa baba alikuwa na mke wa kwanza ana watoto wakubwa na akaoa mwingine, akazaa watoto wengine.”

“Baba yao alisema nyumba ni ya familia na kwa sababu aliacha mtoto mdogo hawa wakubwa wa kike wakae wapumzike mpaka watakapoolewa.”

Naye, Balozi wa Mtaa wa Onjavutiani, Kata ya Sinoni, Arusha, Praygod Mhando, alisema alipigiwa simu na kuelezwa Mandela ameshambuliwa na ndugu zake wawili nyumbani na baadaye alipelekwa hospitali kwa matibabu na kufariki dunia.

“Tulikwenda polisi na majirani wawili kutoa taarifa na polisi walikwenda eneo la tukio, walioshuhudia tukio hilo walisema kwamba walikuwa na ugomvi wa kifamilia kwa sababu ya nyumba ya baba yao walikuwa wakiigombania,” alisema.

Alisema msiba wa mwisho ambao ulifanyika hapo nyumbani ulikuwa ni wa mama yao na kwamba waliumaliza vizuri bila tatizo na kama mtaa hawakujua kama kulikuwa na matatizo mengine kwenye familia hiyo.

“Mandela alikuwa amelala chumbani ndugu zake wa kike wakaja wakamwambia kwanini unalala kwenye chumba cha baba wakati hujaruhusiwa kulala humo, ndipo ugomvi ulipoanza,” alisema.

Habari Kubwa