Watuhumiwa sugu ujambazi auawa Dar

07Nov 2019
Mary Geofrey
Dar es Salaam
Nipashe
Watuhumiwa sugu ujambazi auawa Dar

JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, limewaua watu wawili wanaodhaniwa kuwa ni majambazi sugu, akiwamo aliyefahamika kwa jina la ‘Kambale’ ambaye alikuwa akitafutwa kwa muda mrefu.

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, picha mtandao

Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Lazaro Mambosasa, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na wanahabari na kusema kuwa ‘Kambale’ alijipatia umaarufu wa jina hilo kwa sababu alikuwa akikamatwa na kutoroka.

“Tunawashukuru Watanzania wanaendelea kutoa taarifa za uhalifu kwa Jeshi la Polisi, usiku wa kuamkia leo (jana) tumekamata pisto (bastola) moja na majambazi wawili waliokuwa wakiwahangaisha wananchi,” alisema Mambosasa na kuongeza:

“Wameangushwa chini (wameauawa). Mmoja alikuwa akijiita Kambale kutokana na kuwaponyoka askari kila alipokamatwa, ametesa sana wakazi wa Madizini, Ukonga na maeneo mengine.”

Aliongeza kuwa ‘Kambale’ alikuwa akishirikiana na wenzake wanakodi pikipiki, wanaielekezea sehemu alipo ‘Kambale’, wakifika alikuwa anawachoma kisu na kukimbia na pikipiki.

“Amekuwa akiwateka na kuwaua madereva bodaboda, kila alipokuwa akikamatwa anateleza na kuwatoka askari kama vile samaki aina ya Kambale, lakini mwisho wake na yeye ametangulia mbele za haki,” alisema Mambosasa.

Mbali na hilo, Mambosasa alisema jeshi hilo limeimarisha ulinzi katika maeneo yote ya jiji hilo, wakati wanapotarajia kupokea wageni wanaoshiriki mkutano wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (Sadc) unaotarajiwa kufanyika kuanzia kesho jijini Dar es Salaam.

Mambosasa aliwatahadharisha wakazi wote wa jiji hilo kuwa endapo watafanya utapeli kwa wageni hao sifa itakayobebwa ni ya Watanzania wote na kwamba Jeshi hilo halipo tayari kuona sifa ya Tanzania inachafuliwa.

“Tumejipanga na doria zinaendelea mtaani kwa ajili ya kikao cha Sadc, wageni wetu wanaoingia kuanzia Airport (uwanja wa ndege), mahali watakapofikia hadi kwenye kikao watakuwa salama,” alisema na kuendelea:

“Fukwe zote na eneo la mkutano tumehakikisha usalama upo. Kila mmoja anatakiwa awe mlinzi wa mwenzake, wanaofanya ujanja ujanja toeni taarifa, tutawashughulikia, tusikubali mtu mmoja akachafua sifa ya nchi yetu.”

Habari Kubwa