Watuhumiwa watano ujambazi wauawa

02Mar 2021
Na Mwandishi Wetu
Dar es Salaam
Nipashe
Watuhumiwa watano ujambazi wauawa

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, limewaua watu watano wanaotuhumiwa kuwa ni majambazi na kukamata bastola aina ya STAR iliyokutwa namba ikiwa na risasi tatu ndani, kasha na maganda mawili ya risasi yaliyotumika.

Kamanda wa Kanda hiyo, Lazaro Mambosasa, aliyasema hayo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari na kwamba watu hao waliuawa Jumamosi saa 12:00 asubuhi maeneo ya Kivule kwa Iranga.

Alisema Jeshi la Polisi kupitia kikosi chake cha kupambana na ujambazi liliwaua watu hao waliokuwa kwenye gari namba T 836 DHF aina ya Toyota Noah.

"Majambazi wapatao sita wakiwa kwenye gari hilo wakiwa wanakwenda kufanya uhalifu maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam, kabla hawajatimiza lengo lao, kikosi kazi cha Jeshi la Polisi kiliweka mtego na kufanikiwa kuzuia ujambazi huo kwa kutaka kuwakamata wahalifu hao, lakini majambazi hao walitoka kwenye gari na kuanza kukimbia huku wakiwarushia askari risasi na hatimaye askari walijibu mapigo na kuwapiga risasi watu watano ambao walifariki dunia papo hapo," alisema.

Kamanda Mambosasa alisema mmoja kati ya watuhumiwa hao alifanikiwa kukimbia huku akifyatua risasi ovyo na kumjeruhi askari mmoja.

"Baada ya kuwapekua walikutwa na bastola moja ikiwa na risasi tatu ndani ya magazine na maganda mawili ya bastola. Miili ya marehemu imeifadhiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)," alisema.

Katika tukio lingine, kamanda alisema operesheni iliyofanyika siku mbili kuanzia Jumapili, kuwasaka wezi wa pikipiki imewakamata watu 10 na pikipiki 16.

Kamanda Mambosasa aliwataja baadhi yao waliokamatwa kuwa ni Stephen Paul (38), mkazi wa Ulongoni A, Salum Mustafa (28), mkazi wa Kigogo na Nsajigwa Kaisi (25), mkazi wa Mongo la Ndege A.

"Operesheni hii ilifanyika baada ya kupokea taarifa toka kwa walioibiwa pikipiki zao katika matukio haya ambayo yamekithiri maeneo mbalimbali Dar es Salaam," alisema.

Alisema watuhumiwa hao wamekuwa wakiiba pikipiki katika maeneo mbalimbali Dar es Salaam na kuzipeleka kwa madalali ambao huziuza.

Habari Kubwa