Watumiaji bangi waongezeka

25Jul 2021
Gwamaka Alipipi
Dar es Salaam
Nipashe Jumapili
Watumiaji bangi waongezeka

WATUMIAJI wa dawa za kulevya aina ya bangi nchini wameongezeka, huku uingizaji wa dawa kutoka nje ya nchi ukiwa umedhibitiwa kwa asilimia 95.

Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Vijana na Ajira, Tixon Nzunda, alibainisha hayo jana jijini Dar es Salaam alipotembea Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na  Dawa za Kulevya (DCEA).

Nzunda alisema DCEA imejitahidi kwa asilimia kubwa katika kupambana na kudhibiti uingizaji na matumizi ya dawa za kulevya kutoka nje ya nchi, lakini bado kuna tatizo kubwa la matumizi na ulimaji wa bangi.

Nzunda alisema: "DCEA tangu imeanzishwa, wamejitahidi kuimarisha mifumo ya kisera na kikanuni. Serikali tumekuwa tukiwapa ushirikiano mkubwa katika mapambano ya dawa za kulevya.

'Katika mafanikio hayo, wamefanikiwa kudhibiti asilimia 95 ya dawa za kulevya zitokazo nje ya nchi kuingia nchini."

Nzunda alisema licha ya mafanikio hayo, watumiaji wa dawa za kulevya aina ya bangi bado ni wengi na idadi inaongezeka kwa kasi, hivyo jitihada zinahitajika za kuanzisha vita dhidi ya kilimo cha bangi.

Kamishna Jenerali wa DCEA, Gerald Kusaya, alisema kuanzia mwaka 2013 hadi 2014 kabla ya kuanzishwa kwa DCEA, uingizaji wa dawa za kulevya aina ya heroin nchini ulikuwa ni wa asilimia 88, lakini baada ya mamlaka kuanzishwa mwaka 2015 na kuanza kazi mwaka 2017, kiwango cha uingizaji wa dawa za kulevya aina hizo kilishuka hadi asilimia tano.

"Tatizo la matumizi ya bangi bado lipo juu na linaongezeka, hadi sasa tumekamata milioni ya kilo za bangi, operesheni tunaziendesha kila siku lakini tatizo bado lipo kulinganisha na dawa za kulevya kutoka nje ya nchi ambazo tumezidhibiti," alisema.

Habari Kubwa