Watumiaji wa dawa kuzuia hedhi hatarini

09May 2022
Elizabeth John
NJOMBE
Nipashe
Watumiaji wa dawa kuzuia hedhi hatarini

WATAALAMU wa afya wametoa angalizo kwa wanawake wanaotumia dawa za kuzuia hedhi pasi na ushauri wa daktari kwamba wako hatarini kupata madhara, yakiwamo maradhi ya moyo.

Katika mazungumzo maalum na Nipashe ofisini kwake mjini hapa jana, Shomari Masenga, Daktari wa Magonjwa ya Kinamama Hospitali ya Rufani Mkoa wa Njombe, alitaja dawa hizo kuwa zimegawanyika katika makundi matatu Primolut Tables, Ergometrine Injection na Combined Oral Contraceptive pill.

Akifafanua zaidi matumizi ya dawa hizo, daktari huyo alisema Primolut Tables ni dawa wanazopewa wanawake ambao wanatoka damu nyingi na wamepoteza mpangilio wao wa kuingia hedhi.

"Inatengenezwa na 'component' ya projestine ambayo inafanya kazi ya kupunguza uzito kwenye ukuta wa ndani wa mfuko wa uzazi ambao ukipungua ndiyo damu inatoka nyingi.

"Madhara ya dawa hizi ni kubadilisha mzunguko wa hedhi, kukosa usingizi, kuongezeka uzito, kizunguzungu, kukosa hisia za kufanya mapenzi na kuwa na hasira," alifafanua.

Daktari huyo, akizungumzia matumizi ya Ergometrine Injection, alisema ni dawa zinazotumiwa na mama mjamzito baada ya kutoka kwa kondo la nyuma na kupoteza damu nyingi na zinatengenezwa kwa 'component' ya Ergometrine Maleate.

Hata hivyo, daktari huyo alitoa angalizo kuwa dawa hizo sasa hazitumiki hospitalini kutokana na madhara yaliyobainika.

"Husababisha 'heart  attack' (shambulio la moyo) kwa mtumiaji, moyo unaweza ukafa kwa sababu ya kukosa damu, seli za moyo zitashindwa kufanya kazi, kifua kujaa maji hadi kupelekea kifo. Madhara mengine ni kupumua kwa shida," alisema.

Kuhusu Combined Oral Contraceptive Pill, daktari huyo alisema aina hiyo ya dawa ni kwa ajili ya uzazi wa mpango, akifafanua: "Hii inatumika kuchelewesha siku na kutibu kama unavuja damu nyingi. Dawa hizi zinafanya kazi ya kuzuia kutoka kwa damu ya hedhi, mara nyingi dawa hizi wanapewa ambao wanatoka damu kupitiliza pamoja na wanaotaka kuchelewesha hedhi.

"Zimetengenezwa kwa component aina mbili -- Oestrogen na Progestine. Zinafanya kazi gani? Zinazuia upevushaji wa yai, kusababisha ute wa shingo ya kizazi kuwa mzito na mbegu za kiume kushindwa kupita.

"Madhara yake kiafya ni kwamba zinasababisha kutoka damu kidogo kidogo, shida ya moyo, damu kuganda kwa wenye umri kuanzia miaka 35.

"Madhara mengine ya dawa hizi zote ni makubwa kwa sababu yanasimamisha ufanyaji kazi wa vichocheo katika mwili, wengi wanaotumia dawa hizo ni wale ambao wanakuwa na 'matukio'.

"Mtu anakua anataka kwenda kwa mpenzi wake au kwenda sehemu yoyote hataki kuwa kwenye hedhi, basi anakunywa dawa hizi ili kuzuia," Dk. Masenga anafafanua.

Habari Kubwa