Watumiaji wa saruji Dangote njia panda

28Nov 2016
Sanula Athanas
Dar es Salaam
Nipashe
Watumiaji wa saruji Dangote njia panda

KIWANDA cha saruji cha Dangote kilichopo Mtwara, kimesitisha uzalishaji kutokana na kuelemewa na gharama za uendeshaji.

Taarifa za kuaminika kutoka Mtwara ziliiarifu Nipashe wiki iliyopita kuwa kiwanda ambacho ni kikubwa zaidi katika uzalishaji wa saruji nchini, kimesitisha shughuli zake.

Na baada ya kutafutwa na gazeti hili kuzungumzia uamuzi huo mwishoni mwa wiki, Mkurugenzi Mtendaji wa kiwanda hicho, Harpreet Duggal, alisema umetokana na gharama kubwa ambazo zimekuwa zikiwakabili katika kukiendesha.

Alisema wako katika mazungumzo na serikali kuangalia namna ya kuitatua changamoto hiyo na wanatarajia kuendelea na uzalishaji, hata hivyo.

"Tumesitisha kwa muda uzalishaji wa sementi kwa sababu za kitaalamu. Changamoto hii tunaendelea kuitafutia ufumbuzi na tutarejea katika uzalishaji muda mfupi ujao," alisema na kufafanua zaidi:

"Tunakabiliwa na changamoto ya gharama kubwa za uendeshaji na serikali inashughulikia suala letu. Tunatumaini kupata jawabu mapema."

Mwezi uliopita Mkurugenzi huyo alilalamikia uamuzi wa serikali wa kupiga marufuku kiwanda chake kuingiza makaa ya mawe kutoka Afrika Kusini na kutakiwa kutumia ya Liganga ambayo alidai yako chini ya kiwango na yanauzwa kwa bei ghali.

Duggal alililalamikia pia Shirika la Maendeleo ya Petroli (TPDC) kwa kushindwa kuwauzia gesi kwa bei rahisi, wakati inazalishwa mkoani Mtwara kilipo kiwanda chake.

Kushindwa kupatikana kwa nishati hizo mbili, alisema Duggal kumefanya Dangote kutumia lita 200,000 za mafuta ya diseli kwa siku, licha ya ahadi ya serikali wakati wa uwekezaji kuwa kingepata nishati ya umeme kwa bei rahisi.

Kiwanda hicho ambacho pia ni kikubwa zaidi Afrika Mashariki, kilianza uzalishaji mwaka mmoja uliopita na kimesaidia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa bei ya bidhaa hiyo nchini.

MASWALI MATATU
Lakini akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu kuhusu madai ya changamoto ya nishati mwishoni mwa mwezi uliopita, Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo, alisema malalamiko ya mwekezaji huyo hayana ukweli na ni uzushi.
Muhongo alimtaka muandishi wa Nipashe kumuuliza Duggal maswali matatu:

"Je, tumewahi kuwa na kikao cha wazalishaji na watumiaji wa makaa ya mawe ya Tanzania? Je, mlikubaliana na kuweka kamati ya kufuatilia matatizo yenu (watumiaji)? Umeshaenda kwenye kamati kulalamikia bei na ubora wa mkaa?"

Muhogo alisema anachoona ni kwamba Mkurugenzi Mkuu wa Dangote "anakwepa uhalisia ulio kwenye makubaliano ya wazalishaji na watumiaji".

“Watumiaji nao wamo kwenye kamati mbona hilo haliongelei?

"Atujibu maswali."

Waziri huyo pia alitaka Dangote aulizwe "walivyokaa kikao na TPDC kuhusiana na suala la gesi, walikubaliana nini?”
Waziri huyo alisema inashangaza kama wanakaa na kukubalina, halafu mwekezaji huyo anakimbilia kwenye vyombo vya habari kulalamika.

“Kinachoonekana ni uzushi na ubabaishaji wa watu ambao wana maslahi yao ya kuagiza hivyo vitu na hatujui wanapata nini.”

Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TPDC, Kapuulya Musomba, alisema mwishoni mwa mwezi uliopita kuwa shirika lake linauza gesi kwa sheria na taratibu zilizopo na kwamba bei elekezi inapangwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma ya Nishati na Maji (Ewura).

“Inapotokea mtu anataka auziwe juu au chini ya ile iliyopangwa na Ewura, hatuna mamlaka ya kubadilisha," alisema Musomba.

"Mtu anaweza kuongea lolote kwa sababu sisi ndiyo tunahusika na gesi lakini tunafuata taratibu kwa kupeleka maombi kwa Ewura, unatuambia kwa jinsi ulivyoleta maombi yako na utauza bei hii. Hapo ndipo tuliposhindwana na Dangote.”

Alisema bei iliyopo kwa sasa ni dola za Marekani 5.12 "kwa kila ‘MMBTU’".

Kuna wakati Dangote alitaka kuuziwa kwa dola 4.75, alisema Musomba, lakini baadaye aliandika barua kuwa hataki bei hiyo, anataka chini ya dola nne. "Ewura ilishindwa kumtimizia".

Alisema pia walipokea barua kutoka kwa Dangote wakitaka TPDC ihakikishe wanapata umeme wa megawat 25 ifikapo Februari mwakani, na kwamba walikutana nao na kukubaliana kuzalisha umeme wa gesi kwa kiwango hicho kwa kampuni ambayo wameiidhinisha.

“Kuna tofauti kubwa kati ya gesi inayotokana na mafuta ambayo baada ya kutolewa mafuta ni uchafu na gesi asilia," alisema.

"Nigeria gesi ni mabaki ambayo wanaweza kuichoma au kutoa bure kwa kuwa wamerudisha gharama zao kwa kutumia mafuta.”
Mmiliki wa kiwanda cha saruji cha Dangote ni Aliko Dangote, mfanyabiashara tajiri zaidi barani Afrika raia wa Nigeria.

Alisema iwapo TPDC itauza gesi kwa bei anayotaka Dangote, hakutakuwa na faida kutokana na mwekezaji.

“Nimeshakwenda kiwandani kwake, anasema kwa mwezi anapoteza dola za Marekani milioni tatu kwa kutumia mafuta, ukipiga hesabu ya matumizi ya mafuta na gesi kwa bei yetu, matumizi ya gesi yako chini sana.

Tunachofanya ni haki na kwa wema, tunawapenda wawekezaji lakini ni lazima tukubaliane mambo ya msingi,” alifafanua.

Habari Kubwa