Watumishi 190,000 kupandishwa vyeo

26Apr 2019
Godfrey Mushi
DODOMA
Nipashe
Watumishi 190,000 kupandishwa vyeo

SERIKALI imesema itawapandisha vyeo watumishi 193,166 ambao wamekasimiwa katika ikama na bajeti ya mishahara kuanzia Mei Mosi, mwaka huu.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika.

 

Mpango huo ulitangazwa jana bungeni jijini Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu George Mkuchika, alipowasilisha kauli ya waziri.

“Katika kutekeleza zoezi hili, waajiri wanaelekezwa kwamba kipaumbele cha kwanza kitolewe kwa watumishi wenye utendaji mzuri ambao wanatarajiwa kustaafu hivi karibuni ili waweze kushughulikiwa mapema iwezekanavyo kabla ya kustaafu.

“Kipaumbee cha pili kitolewe kwa watumishi wenye utendaji mzuri waliokaa kwenye vyeo walivyonavyo sasa kwa muda usiopungua miaka minne na kukasimiwa kwenye ikama na bajeti ya mwaka wa fedha 2017/18,” alisema.

Waziri huyo aliwataka waajiri wote nchini kuhakikisha kwamba wanaendesha upandishaji vyeo watumishi stahiki kwa wakati na kwa kuzingatia tange ya taasisi husika, sifa za kimuundo, kuwapo kwa nafasi iliyoidhinishwa katika ikama na utendaji mzuri kwa mujibu wa matokeo ya tathimini ya utendaji kazi (Opras).

Kwa mujibu wa Waziri Mkuchika, waajiri na maofisa wanatakaotekeleza zoezi hilo kinyume cha maelekezo yaliyotolewa na serikali kuhusu upandishaji wa vyeo, watachukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za utumishi wa umma.

“Kama itakavyokumbukwa, zoezi la upandishaji wa vyeo watumishi waliokasimiwa katika ikama na bajeti ya mishahara ya mwaka wa fedha 2015/16 liliahirishwa mwezi Mei 2016 ili kupisha mazoezi ya uhakiki wa watumishi hewa na mishahara batili pamoja na vyeti vya watumishi wa umma.
"Baada ya kukamilika kwa mazoezi tajwa, Rais John Magufuli aliridhia upandishaji vyeo watumishi kwa awamu.

Awamu ya kwanza iliyoanzia Novemba Mosi, 2017, ilihusisha upandishaji na uidhinishaji wa taarifa za watumishi 59,967 ambao taarifa zao za kupandishwa vyeo zilikuwamo kwenye mfumo wa taarifa za kiutumishi na mishahara (HCMIS), lakini zilikuwa hazijaidhinishwa wakati wa usitishaji tajwa hapo Mei, 2016.

"Awamu hiyo ya pili iliyoanza Aprili Mosi, mwaka jana, ilihusisha watumishi zaidi ya 53,553 ambao walipandishwa vyeo lakini taarifa zao zilikuwa hazijaingizwa kwenye mfumo wakati wa zuio tajwa."Uidhinishaji wa taarifa za watumishi 113,520 kwenye makundi haya mawili kupitia mfumo wa HCMIS umekamilika," Mkuchika alisema.

Habari Kubwa