Watumishi ardhi wabanwa kujieleza

13Jan 2020
Munir Shemweta
Njombe
Nipashe
Watumishi ardhi wabanwa kujieleza

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, ameagiza wakuu wote wa Idara za Ardhi, Halmashauri za Mkoa wa Njombe kuandikiwa barua za kujieleza kutokana na kushindwa kusimamia uingizaji taarifa za viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki wa ukusanyaji kodi ya serikali.

NAIBU Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Angeline Mabula, picha mtandao

Aidha, alitoa miezi mitatu kuanzia Januari 11, hadi Aprili 12, mwaka huu, kwa halmashauri za mkoa wa Njombe kumpatia taarifa ya kuingizwa viwanja vyote vya wamiliki wa ardhi kwenye mfumo wa kielektroniki katika mkoa huo.

Mabula alitoa agizo hilo jana katika kikao chake na watendaji wa sekta ya ardhi wa halmashauri sita za mkoa wa Njombe akiwa katika ziara yake ya kukagua utendaji kazi wa sekta ya ardhi pamoja na kukagua miradi ya ujenzi inayotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa (NHC).

Wakuu wa idara ya ardhi walioangukia mikono ya Mabula kuhusiana na kuandika barua za kujieleza ni kutoka Halmashauri za Njombe Mji iliyoingiza viwanja 7,301, Makambako 5,712, Njombe Wilaya 326, Wanging’ombe 375, Makete 2,156 na Ludewa viwanja 3,793.

Uamuzi wa Naibu Waziri unafuatia kuelezwa kupitia taarifa ya mkoa wa Njombe pamoja na zile za halmashauri zote za mkoa huo kuwa, kuanzia kipindi cha Julai hadi Desemba 2019 ni viwanja 19,645 tu ndivyo vilivyoingizwa kwenye mfumo kati ya viwanja 40,961.

Kwa mujibu wa waziri huyo, utaratibu wa kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki ulianza mwaka 2017, lakini cha kushangaza hadi kufikia sasa zipo baadhi ya halmashauri hazijaunganishwa.

Alisema, kuingiza viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki siyo tu unarahisisha kutambua wamiliki wote wa ardhi, bali unasaidia kuwafuatilia wamiliki wanaokwepa kilipa kodi ya ardhi jambo alilolieleza lisiposimamiwa kwa umakini litapunguza wigo wa ukusanyaji maduhuli ya serikali kupitia kodi ya pango la ardhi.

“Uingizaji viwanja kwenye mfumo wa kielektroniki ulianza tangu mwaka 2017, lakini bado hakuna kilichofanyika hatuwezi kulea uozo huu unaoweza kuwapa mzigo wateja kutokana na malimbikizo ya kodi,” alisema Mabula.

Mabula alisema wizara yake inataka kuwa na malengo yanayoendana na kasi ya serikali ya awamu ya tano na kuiagiza Ofisi ya Ardhi ya Kanda kupitia takwimu za viwanja vilivyo katika mfumo kwa halmashauri za mkoa wa Mbeya na kusisitiza haiwezekani kuwa na Ofisa Ardhi Mteule ama Mkuu wa Idara ya Ardhi asiyefuatilia na kusisitiza katika suala hilo wizara yake haitakuwa na msamaha.

Kuhusu ukusanyaji wa kodi ya ardhi, waziri huyo alionyesha kutoridhishwa na makusanyo ya kodi hiyo kwa halmashauri za mkoa wa Njombe na kwamba kufikia Desemba 2019 halmashauri zote zilikusanya jumla ya Sh. 369,863,643.34.

Alisema kiasi hicho kiko chini ya asilimia 50 ya makusanyo ya kodi ya ardhi katika mkoa huo uliokuwa na lengo la kukusanya Sh. bilioni 1.2.

Katika hatua nyingine, waziri huyo alikagua maendeleo ya ujenzi wa jengo la ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Wanging’ombe unaotekelezwa na Shirika la Nyumba la Taifa kwa gharama ya takriban Sh. bilioni 2.7.

Mabula mbali na kuridhishwa na ujenzi wa jengo hilo amelitaka NHC kuhakikisha jengo hilo linakamilika mapema iwezekanavyo kwa kuwa lilichelewa kukamilika kutokana na changamoto mbalimbali.

Habari Kubwa