Watumishi wa TMDA huru kesi ya bil. 58/-

18May 2022
Grace Gurisha
DAR ES SALAAM
Nipashe
Watumishi wa TMDA huru kesi ya bil. 58/-

WATUMISHI watano wa Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba (TMDA) wameachiwa huru na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu baada ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP) kuwasilisha nia ya kutokuendelea na kesi dhidi yao.

Watumishi hao ni Charys Ugullum, Raymond Wigenge, Ezekiel Mubito, Adelard Mtenga na Abdallah Juma, ambao walikuwa wakikabiliwa na mashtaka ya kuisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. bilioni 58.3 kwa kujilipa posho.

 

Wakili wa Serikali kutoka Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Hassan Dunia, alidai jana mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Ritha Tarimo, kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kusikilizwa kwa mashahidi wa upande wa mashtaka.

"Lakini DPP amewasilisha maombi ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai," alidai Dunia.

Kufuatia taarifa hiyo Hakimu Tarimo alikubaliana na ombi la upande wa mashtaka kwa kufuta kesi hiyo ya uhujumu uchumi namba 5 ya 2018 na kuwaachia huru washtakiwa hao.

Katika kesi ya msingi inadaiwa kati ya Mei na Desemba, 2016 katika Ofisi za Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA wakati huo) kwa sasa TMDA washtakiwa waliisababishia mamlaka hiyo hasara ya Sh. 58,390,000.

 

Ilidaiwa fedha zilikuwa ni posho za wafanyakazi waliokuwa wamesaini malipo yao jambo lililosababisha kujilipa mara mbili. Katika kesi hiyo, shahidi mmoja pekee ndiye aliyekuwa ametoa ushahidi wake.

Habari Kubwa